|
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Humphrey Polepole amesema wabunge wa upinzani wanaotaka kujiunga na
chama hicho tawala mwisho wa kufanya hivyo ni Desemba, 2018
Polepole amesema mwaka 2018 ndio
mwisho wa chaguzi ndogo za ubunge, wale watakaoshindwa kuhamia CCM wabaki
walipo
Polepole ametoa maelezo hayo leo
Jumapili Oktoba 7, 2018 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter
huku baadhi ya watu wakikosoa kauli yake hiyo, wakibainisha kuwa CCM
kimepoteza umaarufu
“Tumezingatia na tunaweka jitihada
zetu zote katika kushughulika na utatuzi wa shida za watu wetu wa Tanzania.
Mwaka 2018 ndiyo mwisho kwetu kufanya chaguzi ndogo za ubunge kwa wale
wanaohama vyama vyao na kujiunga na CCM. Watakaoikosa raundi hii mbaki
hukohuko tutakutana 2020.”
Wakati Polepole akieleza hayo,
hadi sasa wabunge saba wa upinzani wamevihama vyama vyao na kujiunga na CCM,
akiwemo mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Ole Millya aliyejiunga CCM leo
Wabunge hao ni Maulid Mtulia
(Kinondoni), Dk Godwin Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara
(Ukonga). Wanne hao walipojiunga CCM walipitishwa kuwania ubunge na kuibuka
na ushindi
Wengine ni Zuberi Kuchauka
(Liwale) ambaye pia amepitishwa na CCM kuwania ubunge katika jimbo hilo
kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba 13, 2018. Mwingine ni Marwa Chacha
aliyekuwa mbunge wa Serengeti kwa tiketi ya Chadema
Wamkosoa Polepole
Henry Kileo ni baadhi ya waliojibu
ujumbe huo wa Polepole na kusema; “Hiyo project yenu ya ununuzi wa wanasiasa
imewashikisha adabu kwa kuwaonyesha msivyochaguliwa zaidi ni kupora. Katibu
Mkuu wenu kaweka hadharani mambo yote, hamna uhalali wa kisiasa kuongoza.
Sijui unazungumziaje kauli hiyo ya Boss wako.”
Joseph Mauki amesema, “nini
mantiki ya Tweet kama hii kwa kiongozi kama wewe? Wahame haraka haraka ambao
wameshapokea gawio au wafanye mpango wa kuchukua fomu kwako kwa
watakaohitaji?”
Marwa Aruni amesema, “nyinyi
hamshughulikii shida za wananchi bali biashara za siasa. Tangu tupate uhuru
hatujawahi kufanya chaguzi za kijinga kama hizi ambazo zimetafuna robo ya
pato letu. Tumechoka ndio maana hatuendi kupiga kura. Naungana na katibu mkuu
wenu kuwa hamna uhalali kutawala.”
|
Wabunge wanaotaka kuhamia CCM mwisho Desemba 2018
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 07, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 07, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment