Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu habari zilizochapishwa katika Gazeti la
Tanzania Daima la tarehe 26 Oktoba, 2018 toleo namba 4979 na toleo namba 4982
la tarehe 30 Oktoba, 2018 zenye vichwa vya habari “Madudu yaibuka TRA”
na “Barua za madudu TRA zavuja”. Habari inayofanana na hizi, ilisambazwa
pia katika baadhi ya Mitandao ya Kijamii ikiwa na kichwa cha habari "PCCB
Tanzania, to investigate the two tax collectors TRA and ZRB".
Habari hizi zinadai kuwa, Mfumo wa
Ulipaji Kodi kwa Njia ya Kielektroniki – Electronic Revenue Collection System
(e-RCS) umezimwa na kuhujumiwa na baadhi ya Maofisa wa Serikali kwa lengo la
kujinufaisha na kuzorotesha juhudi za ukusanyaji mapato ya Serikali.
Ukweli ni kwamba, mfumo huo
haujahujumiwa wala kuzimwa isipokuwa kuna maboresho ya kiufundi ambayo
yanaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa, unakidhi malengo
yaliyokusudiwa.
Katika kipindi hiki ambacho
maboresho yanaendelea kufanyika, Kampuni za Simu pamoja na Benki mbalimbali
zinaendelea kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na hakuna upotevu wowote wa mapato
kama ilivyoripotiwa na Gazeti la Tanzania Daima na baadhi ya Mitandao ya
Kijamii.
TRA inapenda kuuhakikishia umma
kwamba, hakuna Ofisa yeyote wa Serikali mwenye nia ya kuhujumu mfumo huo kwa
lengo la kujinufaisha na kuzorotesha juhudi za Serikali za ukusanyaji wa
mapato.
Mamlaka ya Mapato Tanzania inatoa
wito kwa vyombo vya habari, wachapishaji, wahariri na waandishi wa habari
kufanya utafiti wa kina kabla ya kuandika habari na kuzingatia weledi wakati
wote wanapotimiza majukumu yao ili kuepuka upotoshaji.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Imetolewa na:
Richard M. Kayombo
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA
MLIPAKODI
Advertisement
Ufafanuzi Kuhusu Habari ya “Madudu yaibuka TRA” Iliyochapishwa na Gazeti la Tanzania Daima
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 31, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 31, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment