Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeyagawa ‘kimya kimya’
makontena 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yaliyokuwa
yakishikiliwa na mamlaka hiyo
Septemba 5, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa
mamlaka hiyo, Richard Kayombo alieleza kuwa iwapo uamuzi wa kuyagawa makontena
hayo utafanyika, taasisi zitakazogawiwa zitajulikana
Hata hivyo, wakati ikisubiriwa kujulikana kwa taasisi hizo,
Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema tayari makontena yamekwishagawiwa
Makontena hayo ambayo yalikosa wanunuzi katika minada yote
mitatu iliyoendeshwa na kampuni ya udalali ya Yono yalikuwa na samani za viti,
meza na mbao za kuandikia yakidaiwa kodi inayokadiriwa kufikia Sh1.2 bilioni
Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere aliliambia Mwananchi
jana kwamba makontena hayo tayari yamegawiwa
Ingawa hakutaja ni watu gani au taasisi zipi zilizonufaika
na mgawo huo, alisisitiza kuwa yalishagawiwa na angetoa taarifa zaidi baada ya
kupokea orodha kutoka kwa wasaidizi wake
“Siwezi kusema lini yaligawiwa wala ni kina nani waliopata
mpaka nipate orodha kutoka kwa wasaidizi wangu wa forodha, maana hata sasa
ninavyozungumza na wewe sipo ofisini... nadhani tukizungumza kesho (leo)
nitaweza kukupatia orodha kamili ya wale waliogawiwa,” alisema
Hivi karibuni kamishna huyo aliliambia Mwananchi kuwa TRA
ilikuwa inakamilisha mchakato wa kuanza kuyagawa makontena hayo baada ya
kukosekana wanunuzi
Alisema sheria ya kodi ya forodha ya Afrika Mashariki
inaelekeza kuwa mali zinazokosa mnunuzi zinawekewa utaratibu maalumu ikiwamo
ule wa kugawiwa bure
“Inapojitokeza minada yote hakuna mnunuzi aliyepatikana,
kuna utaratibu ulioelekezwa kisheria wa kuziondoa mali hizo sehemu ya mnada na
moja ya utaratibu huo ni kugawa bure,” alisema
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja tarehe ya kuondolewa kwa
makontena hayo mbali ya kusisitiza kuwa ofisi yake imeanza kutekeleza taratibu
zinazotakiwa
Alipoulizwa kwa nini makontena hayo yamekosa wateja katika minada
yote, kamishna huyo hakuwa na jibu la moja kwa moja na badala yake alihoji,
“Mimi sijui kwa nini, labda nikuulize wewe maana mnazunguka huku na kule
unaweza kujua.”
Baadaye alipoambiwa huenda hali hiyo inatokana na kiwango
kikubwa cha bei kilichowekwa ambacho kiliwahi kulalamikiwa na wanunuzi, Kichere
alijibu, “Gharama au bei zinawekwa kisheria. Hizi bei hatuzipangi tu kienyeji,
kuna vitu vingi vinaangaliwa kabla ya kuwekwa, mfano kuna gharama ya ardhi,
gharama ya kuhifadhi mzigo na mengineyo. Hizi bei zipo kwa mujibu wa sheria.”
‘Sinema’ ya makontena hayo Kwa mara ya kwanza makontena hayo
yalianza kupigwa mnada Agosti 25, lakini yalikosa wanunuzi kutokana na wateja
wengi kushindwa kufikia bei iliyotakiwa, baadhi yao wakitaja Sh10 milioni kwa
kontena badala ya Sh60 milioni iliyotakiwa
Baada ya makontena hayo kutouzika, Agosti 26, Makonda alitoa
onyo akiwa mkoani Kagera kuwa mtu atakayeyanunua atalaaniwa yeye (mnunuzi) na
uzao wake
Agosti 27, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango
alikwenda bandarini kuyakagua na kuwataka viongozi wenzake serikalini
kutathmini kauli zao akiwataka watu wanaotaka kununua samani hizo wasiogope
Akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita Agosti 30, Rais John Magufuli
alipigilia msumari sakata hilo akiwataka viongozi kuwatumikia wananchi bila
kujali kuwa wako kwenye nafasi gani
“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti mkuu wa mkoa
ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi, kwa nini asilipe kodi?” alihoji Rais
Magufuli
“...Sasa ukichukua makontena kule umezungumza na watu
wengine labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako halafu ukasema tena
labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi maana yake nini,” alihoji Rais
Septemba Mosi ulifanyika mnada mwingine, lakini kwa mara
nyingine makontena hayo hayakuuzika kutokana na wateja kushindwa kufikia bei
iliyotajwa. Kadhalika Septemba 8 ulifanyika mnada mwingine bila mafanikio
TRA yagawa makontena ya RC Makonda kimyakimya
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 31, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 31, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment