Waziri Mkuu asema ushirika si pa kupigia dili


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya ushirika wawatumikie wanachama wao ipasavyo na wasidhani hiyo ni sehemu ya kupiga dili

Amesema Serikali itawachukulia hatua kali viongozi wote wa vyama vya ushirika watakaobainika kuhujumu wana ushirika, hivyo amewataka wafanye kazi kwa uaminifu

Ametoa kauli hiyo jana Alhamisi, Agosti 16, 2018 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Chomachankola, mkoani Tabora

Amewataka viongozi wa chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Tabora cha Igembensabo kuhakikisha wanasaidia wakulima kujiunga na huduma ya bima ya afya

Amesema tayari mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanzisha huduma kwa ajili ya wanachama wa vyama vya ushirika ambao wanatakiwa kuchangia Sh75,000 kwa mwaka

Waziri Mkuu amesema wanachama hao wakijiunga na mfuko huo watapata fursa ya kutibiwa bure wao, wenza wao na watoto wanne kwenye hospitali mbalimbali nchini ikiwemo ya Taifa Muhimbili

Pia amewahamasisha wananchi wa wilaya hiyo wajiunge na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupata matibabu wao pamoja na familia zao kwenye hospitali zilizoko ndani ya mkoa Tabora

Katika hatua nyingine, Majaliwa amewataka wakulima wa zao la pamba wajiandae kwa kupanua mashamba yao katika msimu ujao wa kilimo kutokana na uwepo ya masoko ya uhakika

Amesema kwa sasa kuna viwanda vingi vya kuchambua pamba ambavyo vimeanza uzalishaji na baadhi ya wamiliki wake wamelalamikia upungufu wa malighafi

Waziri Mkuu asema ushirika si pa kupigia dili Waziri Mkuu asema ushirika si pa kupigia dili Reviewed by KUSAGANEWS on August 17, 2018 Rating: 5

No comments: