Walimu 24 wapelekwa Jangwani Shule iliyofanya Vibaya


WALIMU 24 wamepelekwa katika Shule ya Sekondari ya Jangwani kuziba nafasi za walimu walioondolewa shuleni hapo kutokana na matokeo mabaya iliyoyapata kwenye mtihani wa kidato cha sita, mwaka huu.

Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu, aliiambia Nipashe kuwa tayari serikali imejipanga kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo kwa kupeleka walimu wapya baada ya kuwaondoa waliokuwapo

Alisema tayari wameondoa walimu 48 na wamepeleka walimu wapya 24 ambao wamewatoa wilaya zote za Jiji la Dar es Salaam. 

Tumeshaanza kupeleka walimu katika Shule ya Jangwani, lakini pia baadhi yao tumewaondoa. Kazi hii ya kutoa na kupeleka walimu inafanywa kwa umakini na utaalamu mkubwa, hatukurupuki. Tunataka kuhakikisha wanaopelekwa ni walimu wazuri," alisema Lissu.

Alibainisha kuwa jumla ya walimu waliokuwapo katika shule hiyo ni 87, lakini ina 63 baada ya baadhi yao kuhamishwa.

Bado tunaendelea kuiimarisha shule hiyo katika maeneo yote, mbali na kuweka nguvu kwa walimu, tumepanga kuimarisha pia usimamizi wa nidhamu kuanzia kwa wanafunzi wenyewe mpaka juu na tunaimarisha ulinzi pia," Lissu alisema. 

Agizo la kubadilisha uongozi na walimu wa shule hiyo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, baada ya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya zaidi katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotolewa Julai 13, mwaka huu. 

Katika agizo lake, Jafo pia alitaka kuondolewa kwa walimu waliokaa muda mrefu shuleni hapo, akiongeza kuwa shule hiyo ilikuwa na sifa kubwa kitaifa na ilikuwa ni ndoto ya kila msichana kusoma hapo. 

Katika matokeo hayo, shule hiyo ilishika nafasi ya 451 kati ya 453 zilizofanya mtihani huo

Walimu 24 wapelekwa Jangwani Shule iliyofanya Vibaya Walimu 24 wapelekwa Jangwani Shule iliyofanya Vibaya Reviewed by KUSAGANEWS on August 16, 2018 Rating: 5

No comments: