Waganda wataka Bobi Wine atendewe haki


Wakati wananchi wa Uganda wakitaka mbunge wa upinzani Robert Kyagulanyi 'Bobi Wine' aachiwe ili apatiwe matibabu ,Rais  Yoweri Museveni amesema mbunge huyo hajajeruhiwa

Katika taarifa yake ya kwanza kuhusu afya ya mbunge huyo aliyekamatwa na vikosi vya usalama nchini, Museveni amevishutumu vyombo vya habari akidai kwamba vinaeneza habari za uongo

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari mbunge huyo ambaye pia ni msanii, ana matatizo ya figo ambayo yanahitaji kutibiwa ipasavyo na madaktari bingwa waliobobea kutoa matibabu sehemu nyeti kama hayo ya ndani ya mwili

''Vyombo vya kueneza habari zisizo za kweli vimekuwa vikitangaza kwamba mjukuu wetu, asiye na nidhamu Wine, ni mgonjwa mahututi, hawezi kuzungumza na mengineyo,'' alisema Museveni

Aliongeza kwamba vyombo vya habari vilisema kwamba  maofisa wa usalama wamemjeruhi vibaya Bobi Wine kwa sababu ya namna walivyokabiliana na wabunge wakati wakiwakamata

Tayari Bobi Wine alishapata matibabu kutoka kwa madaktari wa Arua, Gulu na Kampala. Hakuwa na majeraha ya kichwa, kifua au mifupa kuvunjika, wameniarifu," ilisema taarifa hiyo  ya rais

Museveni pia alilaumu watu maalum ambao alieleza kuwa ni wa nje wanaotafuta kuingilia siasa za nchi hiyo.</p></div><div><p>Chama cha madaktari Uganda kinasema mahali wanapohifadhiwa wabunge wa upinzani na vyombo vya usalama akiwemo Bobi Wine ni pa hatari na panaweza kuwasababishia vifo
Viongozi wa chama hicho walisema madaktari wa Jeshi la UPDF hawana ujuzi wa kutosha kutoa matibabu kwa wabunge hao wanaodaiwa kujeruhiwa vibaya na maofisa wa usalama

Wameelezea kuwa wako tayari kushirikiana na UPDF kuwashughulikia wabunge hao na washukia wengine kufuatia ghasia hizo

Rais wa chama cha madaktari, Dk  Edward Ekwaro Ebuku  alisema: ''Ugonjwa wa figo unatakiwa uangalizi wa dharura, jeshi la Uganda limemficha huyu Bobi Wine, isitoshe walimkataza daktari wa familia kumtibu.''

''Sasa hivi hatujui hali yake ikoje. Lakini tunafikiria wamemficha kwa sababu hali yake ni mbaya zaidi,'' alisema

Wataalamu wa afya wanafafanua kuwa mtu akiwa na matatizo kwenye figo ni rahisi sana sehemu nyingine kama maini na ubongo wake kuathirika iwapo hatua za dharura hazichukuliwi kumtibu

Waliongeza kuwa mbunge Francis Zake ambaye ni miongoni mwa waliokamatwa yuko mahututi na anahitaji kuhamishwa kutoka hospitali moja hadi nyingine kupata matibabu ya hali ya juu

Wamejitolea kushirikiana na UPDF kutoa matibabu ili kuyanusuru maisha ya waathirika wote wa ghasia waliojeruhiwa na waliomo katika hali mbaya

'Hatujapata ruhusa kuingia kambi za jeshi kuwaona wabunge hao, tutamuandikia mkuu wa jeshi Rais Museveni ili atupe ruhusa twende tumsaidie huyu mheshimiwa Robert Kyagulanyi', alisema  Ebuku
Juzi  mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi na wengine watano kupata majeraha wakati polisi ilipokuwa ikizima maandamano ya wananchi  wa Manispaa ya Mityana Magharibi mwa Kampala

Vurugu hizo ziliibuka baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa mbunge wa upinzani Francis Zaake amekufa baada ya kupigwa na maofisa wa usalama anakoshikiliwa yeye na wenzake

Msamaji wa jeshi la nchi hiyo Brigedia Richard Karemire aliliambia gazeti la Daily Monitor kwamba mbunge huyo anatibiwa vizuri na hali yake inaendelea kutengamaa

Raia wa Uganda wanaoishi nje ya nchi  wameendelea kutuma ujumbe wa kuishtumu Serikali kwa vitendo vyake vya kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani na raia kwenye mitandao ya kijamii

Mwanasheria wa mwanamuziki huyo alisema  kwamba Bobi wine amechomwa sindano iliyomfanya asijitambue mpaka muda huu, na hata wanaomtembelea hawatambui wala uso wake hautambuliki  huku masikio na pua zikitoa damu

Alisema  daktari wa jeshi anadanganya  kwamba sindano waliyomchoma ni ya kupunguza maumivu ya  kapigwa

Mwanasheria huyo alisema  mwenye hotel ambako Bobi wine alikuwa anakaa alisema  hajawahi kuona bunduki eneo lile , na pia kuna  utaratibu wa kuwakagua wateja hivyo vyombo vyao vinaonesha Bobi wine hakuingia na bunduki

Pia akasema baada ya kukamatwa Bob wine, wanajeshi sita waliingia hotelini baadae na hawakutaka kukaguliwa wakati wa kuingia
Mkewe amlilia aandika waraka

Mke wa Bobi Wine, Barbie Kyagulanyi alisema kwenye waraka wake  kwamba alifanikiwa kumuona mume wake akiwa katika gereza la jeshi la Makindye akiwa katika hali mbaya

Alisema kwamba  alifika gerezani hapo akiwa na watu wa haki za binadamu,mwanasheria wake na akamuona mume wake huyo akiwa hai licha ya kuwa na hali mbaya hivyo anamuomba Mungu amsaidie apone

''Bobi ameumizwa, anamaumivu makali kila sehemu anatia huruma tumuombeeni hawezi kusimama wala kutembea''alisema

Alisema mume wake anaongea kwa tabu sana,anatoa damu puani anahitaji kupatiwa huduma za kipekee chini ya uangalizi wa daktari wake

EU walaani Umoja wa Mataifa (EU) umekosoa namna maofisa wa Usalama walivyowakamata wabunge hao na raia kwa madai kwamba walipiga mawe msafara wa Rais Museveni

Taarifa ya wanadiplomasia ya Umoja huo waliopo jijini Kampala inataka wote walioshiriki kuwapiga wabunge na raia katika mazingira yanayotajwa kuwa ni ya kinyama kuchukuliwa hatua

Bobi Wine na wenzake sita wamefunguliwa mashtaka ya kutaka kuipindua Serikali ya Rais Museveni kufuatia vurugu zilizotokea siku ya mwisho ya kampeni katika uchaguzi mdogo wilayani Arua,Kaskazini mwa Uganda

Waganda wataka Bobi Wine atendewe haki Waganda wataka Bobi Wine atendewe haki Reviewed by KUSAGANEWS on August 20, 2018 Rating: 5

No comments: