Yakiwa yamepita masaa kadhaa tokea
msanii wa vichekesho nchini, Alhaji Amri Athuman 'King Majuto' kufariki dunia
siku ya jana, Agosti 8 2018 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako
alikuwa akipatiwa matibabu, watu mbalimbali wametoa salamu zao pole kutokana na
kuguswa na msiba huo.
Taarifa ya msiba wa Mzee wa Majuto
umegusa watu wengi kutoka ndani ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania,
kutokana na uhodari na umahiri wa kazi za sanaa alizokuwa akizifanya na
kukubalika kwa jamii yote kuanzia watoto hadi wazee.
Alhaji Amri Athuman alizaliwa mwaka
1948 jijini Tanga na kusoma shule ya Msambweni iliyoko mkoani Tanga mwaka 1959
hadi 1965, ambapo alianza sanaa ya kuigiza kwa mara ya kwanza mwaka 1958 akiwa
kwenye majukwaa mbalimbali.
Katika enzi za uhai wake Mzee Majuto
aliwahi kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu kwa kujitolea akiwa na umri
wa miaka 17, ambapo alipata nafasi hiyo kwa kuteuliwa na aliyekuwa Mkuu wa
Wilaya ya Tanga enzi hizo marehemu Issa Mtambo.
Baada ya kufikisha miaka 18, Mzee
Majuto alichaguliwa kwa mara nyingine kujiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) kambi ya Twalipo iliyopo maeneo ya chuo cha Uhasibu jijini Dar es Salaam
na ilipofika mwaka 1972 aliachana rasmi na masuala ya jeshi na kufanya kazi za
kijamii.
Mzee Majuto ndio msanii wa kwanza
nchini Tanzania kuandaa na kuuza kazi zake za sanaa kupitia mikanda iliyokuwa
inafahamika kwa jina la 'VHS' enzi hizo, na hadi umauti unamfika (kifo)
ameshiriki zaidi ya kazi 89.
Mbali na kipaji cha uigizaji, Mzee
Majuto pia ni mtunzi, mwandishi wa mswada pamoja na muongozaji filamu.
Marehemu Mzee Majuto ni miongoni mwa
wasanii walioweza kufanikisha ndoto za vijana wengi waliokuwa na nia ya kutaka
kufanya sanaa ya kuigiza, na kupitia yeye kwa namna moja ama nyingine waliweza
kufahamika na kufanikiwa yale waliyokuwa wameyakusudia.
Septemba 24, mwaka 2015, Mzee Majuto
alifanikiwa kuenda kufanya ibada ya 'Hija' kwenye mji wa Makka nchini Saudia
Arabia na kunusurika kifo kufuatia ajali iliyotokea ya winchi kuanguka na kuua
zaidi ya watu 109 na kujeruhi mahujaji 816.
Baada ya tukio hilo, Mzee Majuto
ilipofika Mei 2 mwaka 2016 alitangaza rasmi kuachana na kazi ya uigizaji na
kwamba anataka kumtumikia Mungu na kuomba asamehewe makosa kwa yale aliyotenda
nyuma na kutangaza tena nia hiyo mwaka huu 2018 alipotoka nchini India kwa
matibabu.
Jina la Mzee Majuto limeshindwa
kupata thamani halisi ya kutokana na watu wengi walikuwa wanamtumia Mzee huyo
kwa manufaa yao binafsi bila ya hata kumuangalia yeye namna ya kumuwezesha
kiuchumi hususan katika sekta ya kilimo ambapo enzi za uhai wake alikuwa
akipigania sana.
Itakumbukwa mnamo Oktoba 27, 2017,
Waziri wa Habari, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe alikiri mbele ya umma kuwa
Mzee Majuto amedhurumiwa pesa milioni 25 na kampuni ya filamu ambayo jina lake
amelihifadhi na kudai atatumia hata mshahara wake kuhakikisha anawafunga watu
hao.
Mwili wa marehemu Alhaji Amri
Athuman maarufu kama King Majuto unatarajiwa kusaliwa katika msikiti wa
Muhimbili leo asubuhi na kisha kupelekwa katika uwanja wa Karimjee kwa ajili ya
kupewa heshima za mwisho, kabla ya kuelekea Mkoani Tanga kuzikwa katika
mashamba yake.
Pumzika kwa amani mzee Majuto.
Usiyoyajua kuhusu Mzee Majuto
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 09, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment