Mtu
aliyeshuhudia ajali ya moto uliosababisha kifo cha dereva, utingo kujeruhiwa na
magari saba kuteketea katika kituo cha forodha Rusumo wilayani Ngara amesimulia
jinsi tukio hilo lilivyotingisha eneo hilo
Chrispine
Kamugisha akisimulia ajali hiyo alisema ilitokea wakati lori lililokuwa
limebeba dizeli likiingia kwenye lango la kituo cha forodha Rusumo kilichopo
mpakani mwa Tanzania na Rwanda
Kamugisha
alisema lori hilo lilionekana kupata hitilafu kwenye mfumo wa breki hivyo
lililigonga jingine ndipo moto ulipolipuka na kuunguza mengine yaliyokuwapo
eneo hilo.
“Eneo hili
lina mteremko mkali kuingia sehemu ya maegesho,” alisema
Imeelezwa kuwa
dereva wa lori lililobeba mafuta alishindwa kutoka na kwamba, utingo
alijeruhiwa baada ya kuruka.
Moto huo ambao ulizimwa kwa kutumia helikopta
ya Jeshi la Rwanda ulisababisha taharuki eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino
Olomi alimtaja dereva aliyefariki dunia kuwa ni Abdallah Salimu (37) mkazi wa
Dar es Salaam na utingo aliyejeruhiwa ni Haji Mohammed (22) pia mkazi wa Dar es
Salaam
Alisema magari
ya zimamoto kutoka Karagwe yalifika eneo la tukio na kusaidiana na helikopta ya
kijeshi ya Rwanda kuzima moto huo
“Juhudi
zilizofanywa na kikosi cha zimamoto Karagwe na wenzetu kutoka Rwanda kimesaidia
kwa haraka kuepusha madhara zaidi,” alisema Kamanda Olomi
Akizungumzia
tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mntenjele alisema utingo wa gari
lililokuwa limebeba dizeli aliruka na kuumia hivyo alipelekwa katika Hospitali
ya Nyamiaga kwa matibabu
Baada ya moto
kuendelea huku kukiwa hakuna magari ya zimamoto, Mntenjele alisema
waliwasiliana na viongozi wa Rwanda waliahidi kutuma helikopta iliyofika na
kuuzima
Alisema
kukosekana gari la zimamoto wilayani Ngara na hasa kata ya Rusumo ni changamoto
katika kuokoa maisha ya wananchi na mali zao
Wakala wa
Forodha Kituo cha Rusumo, Abdul Shakuru alisema gari lililosababisha ajali ni
mali ya kampuni ya Lake Oil
Alisema magari
mengine yaliyoteketea ni ya kampuni ya Azam yanayosafirisha mizigo kutoka
Tanzania kwenda Rwanda.
Alisema magari yapatayo 60 yaliyokuwapo eneo
la kituo. Kwa siku, kituo hicho huhudumia kati ya magari 80 na 100
yanayosafirisha mizigo kwenda Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC),
huku mengine yakirejea Dar es Salaam
Shakuru
alisema licha ya vituo vya forodha kufanya kazi kwa saa 24 Tanzania na Rwanda,
changamoto iliyopo upande wa Ngara ni kutokuwa na maegesho ya uhakika
Katika kipindi
cha miaka mitatu, alisema tukio hilo ni la sita
Eneo
palipotokea ajali ni umbali wa kilomita 40 kutoka Rusumo hadi makao makuu ya
Wilaya ya Ngara na kilomita tatu kuingia kituo cha forodha upande wa Rwanda
Kituo hicho
kipo umbali wa kilomita 130 kwenda Karagwe ambako kuna gari la zimamoto.
Simulizi ya moto ulioua dereva na kuteketeza magari saba
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 20, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment