Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema
baadhi ya polisi wanashirikiana na mafisadi kudhulumu ardhi ya wananchi maskini
Amesema mafisadi hao hukimbilia kufungua kesi vituoni
wakilazimisha ardhi iwe mali yao na kuwaonya askari wanaoshirikiana nao katika
dhuluma hiyo
Alisema hayo mwishoni mwa wiki akizungumza na wananchi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ragati kata ya Kasuguti, Bunda
akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo jimboni mwake
Waziri Lugola alisema amepata malalamiko mengi kutoka sehemu
mbalimbali nchini kuwa mafisadi huonea wananchi maskini kwa kupora ardhi
wakidai wao ndio wamiliki. Ili kufanikisha hilo, alisema huwatumia polisi
wasiokua waaminifu kuwakandamiza wananchi
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani jana,
imemkariri Lugola ambaye ni mbunge wa Mwibara akionya wananchi wasikurupuke
kukimbilia kituo cha polisi kufungua kesi za ardhi ambazo hazina uthibitisho wa
jinai
Badala yake, ameagiza kesi au malalamiko yapelekwe katika
mabaraza ya ardhi ya eneo husika ili yatatuliwe kwanza
Alisema mafisadi wanapoona mmiliki halali wa ardhi anagoma
kuondoka eneo husika, hutumia fedha kukimbilia polisi kufungua kesi bila
uthibitisho na askari wasio waaminifu husaidia kufanikisha mwananchi
kunyang’anywa ardhi hiyo
Alisema endapo kesi ya mlalamikaji yeyote ipo mahakamani
anapaswa kuheshimu Mahakama na si kufanya usumbufu katika jamii na kwenda
polisi kutafuta njia ya kumsumbua mwananchi
Lugola alisema endapo mwananchi ana hukumu ya Mahakama
inayoonyesha ameshinda kesi, anapaswa kwenda polisi na nakala ya hukumu
“Rais John Magufuli alianzisha Mahakama ya Mafisadi, kwa
taarifa niliyonayo, ina uhaba wa mafisadi, sasa mimi nitaitafutia wateja kwa
kuhakikisha wale mafisadi ambao huonea wananchi, hutesa wananchi, huiba fedha
za Serikali au taasisi yoyote nitawafikisha katika mahakama hiyo, hatutakubali
unyanyasaji wa aina yoyote,” alisema Lugola akiapa kwamba hatacheka na
mafisadi, bali atapambana nao na yupo tayari kwa lolote
Lugola alisema ameanza kupambana na mafisadi ndani ya wizara
na tayari wameanza kurudisha fedha za Serikali
Mwanzoni mwa mwezi huu akizungumza na waandishi wa habari,
Lugola alisema kampuni saba zinazodaiwa kufanya ufisadi wa Sh28.5 bilioni
katika mradi wa mfumo wa utambuzi uliokuwa ukitekelezwa na Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (Nida), zimeanza kurejesha fedha
Ufisadi huo uligundulika katika ukaguzi uliofanywa na
Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Februari 2016.
Alisema miongoni mwa kampuni hizo, BMTL imekwishamalizana na
Serikali kwa kurejesha Sh569.1 milioni ilizokuwa inatakiwa kulipa
“BMTL hawa Nida walikuwa wamepanga katika jengo lao la
Victoria, lakini kwa muda mrefu walidanganya kuwa eneo ambalo Nida wamelipanga
ni mita za mraba 2,201, lakini ikaja kubainika kuwa vipimo ni vya udanganyifu.
Ilikuja kubainika eneo lililopangishwa lina ukubwa wa mita za mraba 1947,”
alisema
Lugola alizitaja kampuni nyingine ambazo aliagiza zifike
mjini Dodoma na fedha zinazotakiwa kurejesha kwenye mabano kuwa ni Gotham
International (Sh2.8 bilioni), Iris Corporation Berhard (Sh22.9 bilioni),
Gwiholoto Impex (Sh946.4milioni), Skyes Travel Agent (Sh6 milioni), Dk Shija
Paulo Rimoy (Sh27 milioni) na Aste Insurance (Sh 1.2 bilioni).
Lugola aonya polisi kushirikiana na mafisadi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 20, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment