Serikali yatoa neno Watanzania kuajiriwa nje ya nchi


Serikali imekiri bado haina uwezo wa kuwazuia Watanzania waliosomeshwa kwa fedha za Serikali kuajiriwa nchi nyingine licha ya uhaba wa wataalamu wa mafuta na gesi kuwapo nchini

Akizungumza leo Agusti 20, 2018, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk Khamisi Mwinyimvua amesema kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kuwazuia Watanzania kufanya kazi kwenye kampuni zilizopo nje ya nchi

"Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kutoa ufadhili kwa wanafunzi na lengo ni kuongeza wataalamu ili kukidhi mahitaji, lakini ni vigumu kumzuia mtu asiende kufanya kazi sehemu nyingine," amesema Mwinyimvua wakati wa hafla ya kuwaaga wanafunzi 20 watakaokwenda nchini China kusoma mwaka huu

Amesema  jumla ya watanzania 100 wamepelekwa China kwa ajili mafunzo maalumu kwenye sekta ya mafuta na gesi huku changamoto ikiwa ni jinsi gani nchi inanufaika na wataalamu hao

Amesema kwa kiasi kikubwa kazi za uvunaji mafuta na gesi zinaendeshwa na kampuni binafsi hivyo inashindwa kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wazawa

Hata hivyo, amesema kupitia sheria ya ajira imeweka msisitizo kwa kampuni za kugeni kuajiri Watanzania wengi ili kunufaika na rasilimali za ndani

"Ni fedha nyingi zinapotea kwa kukosa wataalamu kwa sababu Watanzania sio wengi kwenye sekta hii," amesema

Aidha amesema kupitia mpango wa kuwasomesha watu nje ya nchi, kutasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu hususan kwenye mafuta na gesi
Naye Naibu balozi wa China,XU Chen amewahimiza wanafunzi hao kuwa wazalendo kwa nchi yao hasa katika kukuza sekta ya gesi ambayo ina mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa

"Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali ila bado mnahitaji wataalamu ambao wanaweza kuzalisha kwa maendeleo ya nchi," amesema

Kwa upande wake, Emmanuel Kessy ambaye ni mmoja wa wanafunzi wa shahada ya uzamivu aliahidi kuwa wapo tayari kuitumikia nchi yao kwa weledi mara baada ya kurejea nchini

"Sisi tunakwenda kufanya kazi kwelikweli kwa sababu nchi imetutuma na tukirudi tutatafuta jinsi gani ya kuifanya gesi kuwa biashara yenye manufaa zaidi," amesema

Mpango huo unafanyika chini ya mkataba wa miaka saba kati ya China na Tanzania ulioanza mwaka 2013 ambapo hadi sasa jumla ya watanzania 100 wamenufaika na mafunzo hayo

Serikali yatoa neno Watanzania kuajiriwa nje ya nchi Serikali yatoa neno Watanzania kuajiriwa nje ya nchi Reviewed by KUSAGANEWS on August 20, 2018 Rating: 5

No comments: