Rais John Magufuli amempa pole Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliyepata ajali ya gari leo Jumamosi Agosti 4,
2018 mkoani Manyara na kupata majeraha sehemu mbalimbali mwilini
Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais
Ikulu, Gerson Msigwa inasema kiongozi mkuu huyo wa nchi amemuombea waziri huyo
apone haraka na kuwashukuru madaktari na wauguzi wa kituo cha afya Magugu
walioanza kumpa huduma ya kwanza
Pia, amewashukuru viongozi wa hospitali ya Selian ya
jijini Arusha kwa juhudi walizozifanya kuokoa maisha ya Dk Kigwangalla na
majeruhi wengine wa ajali hiyo
Rais Magufuli ametoa salamu za pole kwa familia, wafanyakazi
wa wizara, ndugu, jamaa na marafiki wote kufuatia kifo cha ofisa habari wa
wizara hiyo, Hamza Temba
Taarifa hiyo inaeleza kuwa leo jioni Rais Magufuli aliungana
na viongozi wa wizara hiyo kumpokea Dk Kigwangalla katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam
Dk Kigwangalla amesafirishwa kwa ndege kutoka Arusha kuja
jijini hapa kwa matibabu zaidi
Inaeleza kuwa waziri huyo amepata ajali katikati ya vijiji
vya Mdolii na Minjingu Wilaya ya Babati mkoani Manyara baada ya gari lake
kupinduka na kusababisha kifo cha Temba huku watu wengine watano akiwemo yeye
kuumia
Akiwa JNIA, Rais Magufuli alikuwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga,
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya
Rais Magufuli ampa pole Dk Kigwangalla
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 04, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 04, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment