NEC Kutumia Nguvu Nyingi Kutoa Elimu Kuhusu Uchaguzi


Wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani zikianza kesho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema itaongeza nguvu ya utoaji elimu kwa vyama vya siasa ili kupunguza malalamiko

NEC imetangaza kuwa Septemba 16 utafanyika uchaguzi katika majimbo ya Monduli mkoani Arusha, Ukonga (Dar es Salaam) na Korogwe Vijijini (Tanga) na uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 21 zilizoko katika mikoa 10 ya Tanzania Bara

Uchaguzi katika majimbo hayo matatu unafanyika baada ya Mwita Waitara aliyekuwa mbunge wa Ukonga na Julius Kalanga wa Monduli, wote kuhama vyama kutoka Chadema kwenda CCM

Waitara na Kalanga wamepitishwa na CCM kuwania ubunge kwenye majimbo yao

Jimboni Korogwe Vijijini uchaguzi unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Stephen Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu kilichotokea Julai 2. CCM imempitisha Timotheo Mzava kuwania ubunge

Wagombea wa Chadema waliopitishwa kuwania ubunge ni, Asia Msangi (Ukonga), Amina Saguti (Korogwe Vijijini) na Yonas Laiser (Monduli).

Hadi jana, ACT-Wazalendo ilikuwa ikiendelea na mchakato wa kuwapata wagombea

Uchaguzi katika kata 21 unafanyika baada ya madiwani wengi kujizulu kutoka vyama vya upinzani na kujiunga na CCM, wengi wakisema wanakwenda kuunga mkono juhudi za maendeleo za Rais John Magufuli

Katika uchaguzi uliopita wa Agosti 12 uliohusisha Jimbo la Buyungu na udiwani kwenye kata 77, yalijitokeza malalamiko yakiwamo ya mawakala kuzuiwa kuingia kwenye vituo na fomu za wagombea kutojazwa ipasavyo

Kwa sababu hizo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia alisema juzi kuwa wamejipanga kupunguza malalamiko na kwamba nguvu kubwa itaelekezwa katika utoaji elimu

“Tutaongeza nguvu eneo la elimu hususan kwa vyama vya siasa ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza kwa kuwa huwezi kuyamaliza,” alisema Dk Kihamia

Alisema wamebaini baadhi ya malalamiko yanatokana na elimu ikiwamo suala la mawakala, ujazaji wa fomu za wagombea akitolea mfano wa dereva ambaye anaweza kusababisha ajali kwa magari mengine ambayo hayakuwa na kosa

“Ni ngumu kuondoa malalamiko yote, ni kama mchezo wa mpira wa miguu, mtu anapofungwa atatoa malalamiko iwe kwa mwamuzi au kwa nani, kwa hiyo tunajitahidi kuongeza elimu ili kupunguza malalamiko,” alisema Dk Kihamia

NEC Kutumia Nguvu Nyingi Kutoa Elimu Kuhusu Uchaguzi NEC Kutumia Nguvu Nyingi  Kutoa Elimu Kuhusu Uchaguzi Reviewed by KUSAGANEWS on August 20, 2018 Rating: 5

No comments: