Afya ya Kigwangala yaimarika,Kutoka Moi Wakati Wowote


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), anatarajiwa kuruhusiwa wakati wowote baada ya afya yake kuimarika.
Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, akiagana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati alipokwenda kumjulia hali katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), jijini Dar es Salaam jana.   PICHA: ANDREW CHALE
Hayo yalibainika jana baada ya Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, kumtembelea kwa mara ya tatu kwenda kumjulia hali waziri huyo ambaye alipata ajali ya gari akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Manyara.

Kikwete alimtembelea Kigwangalla mara ya kwanza Agosti 8, mwaka huu alipokuwa amelazwa katika wodi ya Mwaisela na baadaye Jumatano wiki hii akiwa kwenye wodi maalum MOI.

Jana, Rais mstaafu Kikwete alimjulia hali Kigwangalla na kubadilishana naye mawazo akimtakia afya njema na apate nafuu ili kuendelea na majukumu yake ya kila siku. Kikwete pia alimpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya katika maendeleo ya sekta ya utalii

"Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi, hongera sana," alisema Kikwete wodini hapo.</

Jopo la madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dk. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani na kwamba kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wa kushoto ambao pia unaendelea kuimarika

Hata hivyo, Dk. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake inaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani huku akiendelea na mazoezi

Aidha, juzi jioni, Dk. Kigwangalla alifanya mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya hospitali hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kurejea wodini kwa kupanda ngazi kwa miguu katika jengo anamopatiwa matibabu mpaka gorofa ya sita

Waziri Kigwangalla alipata ajali ya gari Agosti 4, mwaka huu mkoani Manyara akiwa katika ziara ya kikazi akiwa na watu sita, akiwamo Ofisa Habari wa Wizara hiyo, Hamza Temba, ambaye alifariki dunia.
Afya ya Kigwangala yaimarika,Kutoka Moi Wakati Wowote Afya ya Kigwangala yaimarika,Kutoka Moi Wakati Wowote Reviewed by KUSAGANEWS on August 19, 2018 Rating: 5

No comments: