WATOTO WAWILI WAUAWA, WAZAZI WAO KUJERUHIWA KISHA MUUAJI KUJICHOMA KISU .

Watoto wawili wameuawa  na wawazi wao kujeruhiwa kwa kupigwa kwa  nondo na kuchomwa kwa  kisu sehemu mbalimbali za miili yao kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ugomvi wa mahari.

Tukio hilo limetokea jumamosi tarehe 18.8.2018 katika kitongoji cha Machinjioni  kijiji cha Nyang’aranga kata ya mugeta wilayani Bunda ambapo Mwenyekiti wa kitongoji hicho bwana  Mtatiri Irondo , amesema chanzo cha mauaji hayo ni ugonvi wa mahari kati ya  familia ya bwana magoiga mgendi na kitonyi machango.

Ametaja watoto waliouawa kuwa ni Bhoke Magoiga wa miaka sita ,peter Magoiga mwaka mmoja na nusu,huku waliojeruhiwa ni Mary magoiga 36 pamoja na magoiga mgendi mwenye miaka 52 , tukio hilo la kikatili limefanywa na  Kitonyi Machango miaka 52.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho bwana Paul Marwa, amesema kuwa tokio hilo siyo mara ya kwanza kwani tukio kama hilo liliwahi kutokea japo mtuhumiwa hakukamatwa baada ya kutoroka na kutokomea kusikojulikana.

Diwani wa kata ya Mugeta  Mganga Jongora amesema wamelaani kitendo hicho cha kinyama  na kuwasihi wananchi wasijichukulie sheria mikononi kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria  za nchi na haki za binadamu hasa haki ya kuishi.

Aidha kuhusu kutoa elimu ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia diwani huyo amedai kuwa wamekuwa wakitoa mara kwa mara lakini baadhi ya watu bado hawabadiliki kwa kuacha tabia za namna hiyo, hivyo ameisihi serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria ili kuwa mfano kwa watu wengine.

Hata hivyo jeshi la polisi kupitia kwa Mrakibu wa polisi ambae pia ni Mkuu wa polisi wilaya ya Bunda Imilian Kamhanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa muuaji alitenda tukio hilo na kuuwa mtoto mmoja papo hapo huku  wa pili akifariki njiani akipelekwa hospitalini  kupatiwa matibabu

Aidha ameongeza kwamba baada ya mtuhumiwa kutenda tukio hilo alijichoma kisu tumboni hadi utumbo ukatoka nje lakini alisaidiwa na wananchi waliofika katika eneo hilo na kumfunga kitamba sehemu ya jeraha na kwa sasa anapata matibau katika hospitali teule ya bunda DDH akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.

Mrakibu wa polisi Kamhanda amewaomba idara ya ustawi wa jamii kuendelea kutoa elimu katika vijiji mbalimbali ili kupunguza vitendo vya kikatili vinavyoendelea kujitokeza wilayani hapa.
WATOTO WAWILI WAUAWA, WAZAZI WAO KUJERUHIWA KISHA MUUAJI KUJICHOMA KISU . WATOTO WAWILI WAUAWA, WAZAZI WAO KUJERUHIWA KISHA MUUAJI KUJICHOMA KISU . Reviewed by KUSAGANEWS on August 20, 2018 Rating: 5

No comments: