Wakati joto la wapinzani kuhamia CCM likiendelea kuwa juu,
Mbunge wa Mtama kupitia chama hicho, Nape Nnauye amesema suala hilo lina
ukakasi akitaka itungwe sheria itakayosimamia mchakato huo
Nape aliyasema hayo juzi wakati wa mafunzo ya siku mbili ya
kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge na wajumbe wa Tume ya
Utumishi wa Bunge
“Ifikie mahali turuhusu mtu akihama chama, ahame na ubunge
wake au na cheo chake alichonacho,” alisema
“Hii kitu ina ukakasi, ingawa haivunji sheria, lakini ina
ukakasi na kama ina ukakasi ni vizuri tukatengeneza forum (jukwaa) kwa ajili ya
kusimamia sheria za mchezo huo katika mfumo wa vyama vingi.”
Alisema suala hilo ni msimamo wake wa siku nyingi na ni
vyema likaangaliwa kwa kiasi gani linaimarisha demokrasia nchini
Nape alisema ni vizuri kuangalia ni kwa kiasi gani
‘hamahama’ hiyo italinda kura zilizopigwa na wananchi walipomchagua mwakilishi
wao
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, kumekuwapo na wimbi la
madiwani na wabunge wa upinzani kuhamia CCM, jambo lililosababisha kufanyika
uchaguzi mdogo mara nne, wa hivi karibuni ukiwa ni ule wa Agosti 12
Wabunge waliohamia CCM na vyama walivyotoka ni Mwita Waitara
aliyekuwa mbunge wa Ukonga (Chadema); Julius Kalanga (Monduli-Chadema); Dk
Godwin Mollel (Chadema-Siha) na Zuberi Kuchauka (CUF-Liwale) na Maulid Mtulia
(CUF- Kinondoni).
Pia yumo Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) aliyetoka CCM
kwenda Chadema
Hata hivyo, Mollel na Mtulia walipitishwa na CCM kugombea
tena katika majimbo hayo na kushinda, huku Kalanga na Waitara wakiwa tayari
wamepitishwa na chama hicho katika majimbo hayo
Pia aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius
Mtatiro naye amehamia CCM hivi karibuni
Kadhalika ‘hamahama’ hiyo imesababisha uchaguzi mwingine wa
Septemba 16 utakaohusisha majimbo matatu na kata 21
Mbali na Ukonga na Monduli, uchaguzi huo utahusisha Jimbo la
Korogwe Vijijini ambalo liko wazi baada ya mbunge Stephen Ngonyani kufariki
dunia Juni 2
“Kuna wajibu wa chama na wa wapiga kura, hatuwezi kupuuza
wajibu wa wapiga kura, sio tu kwa sababu ni vyama vya siasa, lakini nchi yetu
haina utaratibu wa mgombea binafsi, basi hatuwezi kupuuza wajibu wa wapiga
kura,” alisisitiza Nape
“Yaani wakishapiga kura haturudi kuwauliza chochote, halafu
tunaondoka, halafu tunarudi kwao tena baadaye.”
Nape ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, alisema hilo ni suala la mjadala mpana kwa sababu chama ni
sehemu ndogo ya jamii iliyopiga kura
“Suala hili lina ukakasi na ukakasi wake ni sehemu ndogo,
ipo wapi nafasi ya wapiga kura ambao hawana vyama, wapiga kura ambao walimpigia
mtu bila kujali vyama vyao, nafasi yao ipo wapi. Hii ndiyo hoja.”
Pia, alizungumzia kwa uchache kuhusu sababu za wapinzani
kuhama vyama akisema ni vigumu kujadili sababu za wanaohama, lakini ni kwa kuwa
sababu ni zilezile
“Umefika wakati wa kujadili nafasi ya wapiga kura ambao
waliamua kutoka asubuhi na mapema kwenda kupiga kura bila kujadili vyama vyao,
nafasi yake imeheshimiwa kwa kiasi gani, ipo wapi na inalindwaje,” alisema Nape
Akizungumzia kauli ya Nape, Katibu wa Wabunge wa CCM, Jason
Rweikiza alisema ndani ya chama chao kuna changamoto na vilevile mambo mazuri
Alisema kuwa wapinzani wanaoona huko walipo mambo hayaendi
wanaweza kwenda popote wanapotaka
“Lakini sheria yetu
inasema ukihama chama chochote unapoteza cheo chako, tungekuwa na mgombea
binafsi mambo yangekuwa tofauti,” alisema Rweikiza
Rweikiza ambaye pia ni mbunge wa Bukoba Vijijini, alisema
mtu aliyehama chama kwenda kingine anapoteuliwa kugombea tena uongozi kwenye
chama alichohamia huo unakuwa siyo uamuzi wa mtu mmoja, bali ni ya chama
“Ninatofautiana na Nape kwamba mtu anapohama anakuwa
amewasaliti wapiga kura, kwani chama kinapoamua kumrejesha agombee nafasi
ileile ni kuheshimu wananchi na kutumia haki yao kumchagua tena kama kweli
wanampenda.”
Alisema changamoto anayoiona katika hamahama hiyo ni gharama
za uchaguzi ambazo hata hivyo alidai kuwa ni sehemu ya maisha kwa kuwa gharama
katika maisha haziepukiki
Alitoa mfano kuwa mtu akijenga nyumba nzuri kuna siku
anaweza kukuta rangi imetoka au ina nyufa, lakini hawezi kuacha kuikarabati
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu
alisema maoni ya Nape ni sahihi
“Lazima tuangalie tulipotoka, awali waliohama vyama walihama
kutokana na sababu za msingi, lakini sasa ni kama mchezo wa kuigiza. Tukiacha
haya yaendelee hatutaipeleka nchi pazuri,” alisema Mwalimu
Alisema ni lazima kuwe na utaratibu wa kuwa na chombo cha
kudhibiti hilo na wale wanaotoa sababu za kuunga mkono juhudi wasiruhusiwe
kugombea tena
“Hao wanatuingiza kwenye hasara na hatari kubwa. Labda kama
tutaamua kwamba atakayejitoa, anapewa miaka mitano ndipo anagombea tena pengine
wataheshimu utu na gharama zinazoteketea.”
Mwalimu ambaye aligombea ubunge Jimbo la Kinnondoni mwaka
huu, alisema wapo wanasiasa wenye sababu za msingi za kutoka na hawawezi
kuzuilika.
“Lakini wapo ambao
wanafanya siasa na kudai kuwa wanaunga mkono juhudi za mtu mmoja pekee,”
alisema
Akizungumzia kauli ya Nape, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Kikatoliki Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema ndiyo maana siku
zote Katiba mpya inadaiwa na wananchi kwa kuwa kila kitu kitapata majibu
kupitia Katiba hiyo
Hata hivyo, Profesa Mpangala alisema kama kuna wanaoona
Katiba si kipaumbele chao, hawana budi kuirekebisha sheria ya vyama vingi.
“Lazima tuheshimu uamuzi wa wananchi ambao ndiyo wapiga kura, hatuwezi kuingia
gharama kila kukicha kwa kisingizio cha kwamba mtu anafuata demokrasia,”
alisema
Alisema hali hiyo inaleta vurugu kisiasa na kusababisha nchi
kutoheshimika
“Lazima tuweke utaratibu kuwa mtu akichaguliwa kuwa mbunge
ni lazima akimalize kipindi chake cha miaka mitano. Wabunge, madiwani
wasiruhusiwe kuhama vyama mpaka uchaguzi mwingine. Lakini pia matakwa ya wapiga
kura yaheshimike.”
Aliyekuwa Mbunge wa Liwale (CUF), Kuchauka aliyehamia CCM
hivi karibuni alisema Nape ni mbunge na ana haki ya kupeleka hoja binafsi
bungeni kuhusu suala hilo. “Kingine ni kwamba, Nape ana uwezo wa kupeleka maoni
yake CCM ili yafanyiwe kazi, mimi sijaona shida ipo wapi,” alisema
Alisema jambo la msingi ambalo mbunge huyo alitakiwa kueleza
ni kuwa CCM inafanya kazi nzuri
“Yale yaliyokuwa yanalalamikiwa na wapinzani, sasa
yanafanyiwa kazi ukilalamika unasikilizwa,”alisema
Kadhalika alizungumzia suala la gharama za uchaguzi na
kusema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ina bajeti iliyotengwa kwa ajili ya
chaguzi
“Labda Tume ilalamike kuwa wapo nje ya bajeti, lakini
ninajua wana fungu lao, siwezi kulalamika katika hilo
Nape awacharuka Hama Hama Inayoendelea
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 18, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment