Familia ya Kindamba ya jijini hapa, imegoma kuuchukua mwili
wa ndugu yao, Salum Kindamba aliyefariki dunia wiki iliyopita kutokana na utata
wa ripoti iliyotolewa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuhusu chanzo
cha kifo chake wanachokihusisha na kupigwa risasi na polisi
Juhudi za kuwapata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa
Temeke, Emmanuel Lukula na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Lazaro Mambosasa hazikuzaa matunda jana
Mwananchi lilipowakosa lilimtafuta msemaji wa jeshi hilo,
Barnabas Mwakalukwa aliyeelekeza watafutwe makamanda hao
“Kuhusu suala hilo mtafute kamanda wa Kanda Maalumu
atalishughulikia,” alisema Mwakalukwa baada ya kuelezwa kuwa juhudi za kumpata
Kamanda Lukula zimegonga mwamba mara kadhaa
Akizungumza kwa niaba ya familia, Omary Kindamba alisema
Salum alifariki dunia Agosti 9, akiwa katika baa iliyopo eneo la Jet Rumo na
rafiki zake. “Mashuhuda wa tukio hilo wameona na kutusimulia kila kitu,”
alisema Omary
“Unajua ilikuwa hivi, hawa jamaa (polisi) walikwenda kwenye
baa hiyo na siku hiyo huyu ndugu yetu alikuwa amebeba begi ambalo ndani yake
kulikuwa na Sh9 milioni
“Sasa siku za nyuma ilisemekana kuwa watu walikuwa
wakipendelea kwenda kwenye eneo hilo kwa ajili ya kugawana fedha na polisi
walikuwa wamearifiwa juu ya mwenendo huo na mara kwa mara walikuwa wakifika
kupiga doria.”
Alidai wakati Salum na rafiki zake watatu wakiwa kwenye baa
hiyo ghafla walizingirwa na polisi ambao waliwaamuru kuwa chini ya ulinzi
Alisema ndugu yao hakutii amri hiyo na kuanza kukimbia,
ndipo alipomiminiwa risasi zinazodaiwa kusababisha kifo chake
“Sasa baada ya tukio hilo ndipo tulipofuatilia katika Kituo
cha Polisi Chang’ombe ambako baadaye tulifahamishwa kweli ndugu yetu alikuwa
amefariki dunia na mwili wake ulihifadhiwa Hospitali ya Temeke,” alisema Omary
Alisema taarifa walizopewa kituoni hapo zilieleza kuwa
alikuwa amepigwa na kitu chenye ncha kali na baada ya mabishano na polisi
wakakubaliana kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kuufanyia
uchunguzi mwili wa marehemu. “Siku ya pili tulivyokwenda tukaambiwa amefariki
(dunia) kutokana na mshtuko uliosababishwa na kitu cha ncha kali.”
Alidai familia haikukubaliana na maelezo yaliyotolewa na
madaktari wa Hospitali ya Muhimbili na wamesusa kuchukua mwili wa marehemu hadi
pale watakapopewa taarifa ‘halisi ya kilichosababisha kifo chake’
“Wanasema ripoti imepelekwa polisi Chang’ombe na kule
hawataki kutupatia na sisi tumeamua hatuchukui mwili wa marehemu hata zikipita
siku 40.”
Akizungumzia sakata hilo, Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa
Magonjwa wa MNH, Dk Praxeda Ogweyo alisema kwa kawaida hospitali huandika
ripoti kamili ya kifo (postmortem), lakini ndugu hupewa kibali cha kuzika
ambacho kinakuwa na taarifa kwa ufupi
“Sisi tulitoa kile kibali chenye taarifa fupi, lakini ripoti
kamili tunaipeleka polisi ili mtu ajue sababu ya kifo tuliyoiandika ni lazima
apate ripoti kamili,” alisema Ogweyo ambaye kitengo chake pia huhusika na
uchunguzi wa sababu za vifo
Alisema kwa kawaida kibali huandikwa sababu ya awali ya kifo
na kibali cha mazishi walichopewa ndugu wa Salum kinaeleza kuwa alifariki kwa
mshtuko
Hata hivyo, alisema ripoti kamili inafafanua kwa kina zaidi
juu ya kifo. Dk Ogweyo alisema walichosema polisi kulingana na ripoti yao
ndicho wao (MNH) walichokiandika
Mwananachi jana lilifika nyumbani kwa kaka wa marehemu eneo
la Kipawa na kuwakuta ndugu wakiwa wamekusanyika huku wakiendelea kuomboleza.
Ndugu hao waliendelea kusisitiza kuwa hawapo tayari kuchukua mwili wa marehemu
hadi watakapojiridhisha juu ya mazingira ya kifo chake
“Mwili hatuuchukui mpaka tujue sababu halisi,” alisema mmoja
wa ndugu ambaye hakutaka kutajwa jina lake. Salum ameacha mke na watoto wanne
wakiwamo mapacha wenye umri wa miaka mine
Familia Dar yasusa maiti ya ndugu Muhimbili, yalia na Jeshi la Polisi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 18, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment