Wakati kukiwa na wimbi la wanasiasa kuhama vyama vya siasa
na kuhamia vingine, waziri wa zamani katika Serikali za awamu ya tatu na nne,
Profesa Mark Mwandosya amesema ‘hamahama’ hiyo inatokana na vyama kukosa
itikadi, dira na sera inayotakiwa na jamii
Profesa Mwandosya ameyasema hayo ikiwa ni siku chache tangu
wabunge wawili wa Chadema kujiuzulu nyadhifa na uanachama wao na kuhamia CCM
Wabunge waliohama ni Julius Kalanga wa Monduli na Mwita
Waitara wa Ukonga. Pia wapo madiwani zaidi ya 50 wa CUF, ACT-Wazalendo na
Chadema waliohamia chama hicho tawala hivi karibuni wakidai kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na Rais John Magufuli
Akizungumza Profesa Mwandosya alisema hamahama ya vyama
inatokana na changamoto inayovikabili vyama vya siasa barani Afrika na nchi
zinazoendelea
Pia alisema kuhama huko kwa wanasiasa kunatokana na vyama
kukosa itikadi inayovisimamia, kwa maana ya mwelekeo na dira pamoja na aina ya
jamii ambayo nchi husika zingependa kuijenga
“Akikaa huko (katika chama alichomo), anaamua kurudi na
kupokewa kwa shangwe (katika chama cha awali) mithili ya mtoto aliyepotea
katika vitabu vitakatifu. Na kwa sababu anakohamia wanatafuta kuongeza namba,
basi inaeleweka kwa nini anapokelewa kwa shangwe,” alisema
Profesa Mwandosya alifafanua kuwa katika mazingira hayo ni
vigumu kutoa sababu za msingi za kiitikadi na kiimani za wanasiasa kurudi
katika vyama vya awali, bali mara nyingi ni za kibinafsi zaidi
Alisema kibaya zaidi mwanasiasa anakorudi kuna watu ambao
hata katika mazingira aliyoyaeleza wameendelea kubaki na kukitumikia chama
anachohamia
Alisema watu anaowakuta ndani ya chama husika wanaona
“walioasi” wanarudi na kupanda ngazi haraka
“Jambo hilo limekuwa dhahiri sana baada ya mwisho wa vita
vya baridi kati ya nchi za Magharibi na za Mashariki,” alisema mwanasiasa huyo
aliyewahi kujitosa kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais mwaka 2005
Profesa Mwandosya alisema kujenga aina ya jamii inayotakiwa
kunahitaji ufafanuzi wa itikadi na sera za uchumi zinazoambatana na itikadi
hiyo. Alisema awali sera hizo zilijikita katika ukabaila au usoshalisti
“Na kila nchi zilitafsiri nini maana ya itikadi na sera hizo
katika mazingira yake. Lakini ilivyo sasa, mfumo wa kiuchumi unaongozwa kwa
misingi ya soko. Kinachofanyika ni kujaribu kupata itikadi kutokana na mfumo wa
uchumi badala ya itikadi kuongoza mfumo wa uchumi,” alisema
“Vyama vimejikuta katika ombwe la tafakuri hiyo kiasi cha
kwamba kushika dola kunakuwa ndio msingi wa kuwepo kwa vyama. Kinachotokea ni
kwamba wananchi na wenye nchi hawaoni tofauti za vyama kwa misingi
niliyoelezea.”
Alieleza kuwa kutokana na sababu hizo viongozi na wanachama
wanaweza kuhama wakati wowote kwenda chama chochote
“Kwani bila misingi ya kiitikadi, imani ya msingi haipo na
masilahi yanakuwa kiini cha maamuzi. Katika hali hii mtu anatoka chama kimoja
anaenda kingine, tena kwa jeuri kabisa,” alisema
Aliongeza kuwa, “sina uhakika kwa kuwa wao ni binadamu
wataridhika na hali hiyo. Kwa kawaida, hapo zamani wanaorudi kundini wangepita
kwanza kwenye mafunzo au madarasa ya itikadi ili kuwapima kwanza.”
Alisisitiza kuwa ombwe lililopo linatokana na changamoto ya
kiitikadi inayoendelea na si kwa Tanzania tu, bali nchi nyingi zinazoendelea
Miongoni mwa wanasiasa waliohama vyama vyao katika siku za
karibuni ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro
Nyalandu aliyehamia Chadema
Wengine ni aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid
Mtulia na wa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) ambao walihamia CCM, kisha
wakateuliwa na chama hicho kugombea tena ubunge katika majimbo hayo na kushinda
tena
Mwandosya afunguka watu kuhama vyama vya siasa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 03, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 03, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment