Bosi Twaweza adai Uhamiaji wamemnyang’anya pasipoti


Idara ya Uhamiaji inadaiwa kuishikilia pasipoti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze

Pamoja na hatua hiyo, Eyakuze amewaambia waandishi wa habari leo Agosti 3 kwamba suala hilo halitawayumbisha, bali taasisi hiyo itaendelea na kazi zake kama kawaida

"Niliombwa nifike Uhamiaji na kupeleka pasi, nikatekeleza, lakini mpaka leo sijapata maelezo wala barua ya kwa nini washikilie pasi yangu," amesema Eyakuze

Amesema baada ya pasi ya kusafiria kushikiliwa, aliomba pasi ya muda kwa ajili ya safari ya kwenda Nairobi kikazi lakini pia alinyimwa, "Hatujapata taarifa ya kuwepo kwa kesi mahakamani," ameongeza

Amesema walipokea barua mbili zikihoji kwa nini wasichukuliwe hatua na wakazijibu

Ingawa hakutaka kuingia undani wa baru hizo, Julai 5, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), iliiandikia barua Twaweza ikiitaka itoe maelezo ndani ya siku saba kuhusu utafiti iliofanya wa Sauti za Wananchi bila ya kibali.

Utafiti huo pamoja na mambo mengine umeonesha kushuka kwa uungaji mkono wa wananchi kwa wawakilishi na viongozi waliowachagua

"Hatutishiki kwa kuitwa na kuhojiwa na Serikali lakini tunadhani ni haki yao kuhoji na sisi kama wajibu wetu kuwajibu. Kwa sababu sheria inaeleza wazi ni tafiti tunazofanya,” amesema

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda amesema hana taarifa ya kushikiliwa kwa pasi ya kusafiria ya Eyakuze

"Bado sijapata hizo taarifa, niko nje ya Dar es salaam, nikirudi nitaifanyia kazi," amesema

Utafiti huo pia ulionyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa, utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, Rais anavyotekeleza majukumu yake tangu alipoingia madarakani na uhuru wa kujieleza katika baadhi ya maeneo

Julai 11, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) iliiandikia barua Twaweza na kuitaka kutoa maelezo kuhusu kibali cha kufanya utafiti huo
Bosi Twaweza adai Uhamiaji wamemnyang’anya pasipoti Bosi Twaweza adai Uhamiaji wamemnyang’anya pasipoti Reviewed by KUSAGANEWS on August 03, 2018 Rating: 5

No comments: