Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewakosoa viongozi
ambao wamekuwa na hulka ya kuwaweka rumande watumishi umma na wanasiasa
akisema, “Katika mkoa wangu hutoona huo upuuzi.”
Katika msimamo huo ambao umeungwa mkono na viongozi wa CCM,
Chadema na wanaharakati, Mtaka amesema kuwaweka rumande viongozi hao si njia
sahihi ya kutatua matatizo yanayowazunguka wananchi huku akitaka mamlaka za
kinidhamu ziheshimike na kuzingatiwa na si vinginevyo
Mtaka ametoa kauli hiyo kipindi ambacho wimbi la wakuu wa
wilaya (ma-DC) kuwaweka rumande watumishi wa umma walio chini yao, wabunge na
madiwani kwa tuhuma mbalimbali likikithiri
Kwa kauli hiyo, Mtaka anaungana na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Seleman Jafo; Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu na aliyekuwa waziri wa Tamisemi, George Simbachawene kukemea
matumizi mabaya ya amri hiyo
Kauli ya karibuni zaidi imetoka kwa Waziri Jafo ambaye
akizungumza na wakuu wapya wa wilaya jijini Dodoma alisema tabia hiyo
inasababisha wananchi kuichukia Serikali na kuwaagiza waitumie ilivyokusudiwa
na si kuonea watu, akiwataka kuzisoma sheria zinazowaongoza ili wafanye kazi
kwa weledi
Mei mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wakuu wa
wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kuzingatia mipaka ya madaraka yao
na kuhakikisha hatua wanazochukua katika utendaji wao zinafuata sheria, kanuni
na taratibu katika utumishi wa umma
Aidha, Septemba 25 mwaka jana, Waziri Ummy akizindua majengo
ya wodi ya wazazi na matibabu ya dharura katika Hospitali ya Wilaya ya
Bagamoyo, alikemea wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka ndani watumishi wa umma
kwa makosa ya kitaaluma
Mwishoni mwa wiki, Mtaka akifunga semina ya madakatari wa
mikoa, wilaya na wadau wa sekta ya afya iliyofanyika jijini Dodoma, aliwataka
viongozi kuwalinda watumishi wa ngazi ya chini na kubainisha kwamba Simiyu
hakuna suala la mtumishi kupelekwa rumande
“Sisi ambao ni viongozi katika sekta hii, kwanza tuwalinde
watumishi wetu, mimi nilipokwenda kuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu niliwaambia ma
DC, moja ya jambo ambalo sitaki kulisikia ni mtumishi yeyote wa umma kuwekwa
lokapu,” alisema
Huku akishangiliwa na watumishi hao wa sekta ya afya, Mtaka
alihoji, “Huyo anayemweka ndani mwenzake, ikitokea kinyume chake angefurahia
suala hilo?”
Alisema hakuna aliyezaliwa anajua na kama kuna kiongozi
anaona mtumishi mwenzake hajui ni wajibu wake kumpa mafunzo na si kumchukulia
hatua za kumweka ndani
“Wakati mwingine ukiona matamko ya wanasiasa kule kwenye
maeneo yenu ya kazi unajiuliza hivi huwa anakaa kushauri haya yatokee,
nazungumza ‘with prestige’ (kwa ufahari) kwa sababu katika mkoa wangu hutoona
huo upuuzi,” alisema Mtaka
Akifafanua kauli hiyo jana alipozungumza na Mwananchi, Mtaka
alisema kuna makosa madogo ambayo yanajitokeza ambayo wakuu wa wilaya au mikoa
wangeweza kuyamaliza kwa kufuata taratibu za utumishi wa umma
Alisema kumekuwapo na matukio ya watumishi kuwekwa ndani
yanayoshusha molari kwa watumishi
“Mamlaka ya kinidhamu kwa kila mtumishi zipo na hazipaswi
kupuuzwa, zipo namna ya kufanya daktari, mwalimu, ofisi elimu, polisi
wanapokosea lakini si kupelekwa polisi,” alisema Mtaka
“Hivi baada ya kumweka ndani na kutoka kipi kinafuata?
Ukitumia mamlaka vibaya huwezi kupata matokeo,” aliongeza, “Kama ni kiongozi
unasimamia misingi ya utumishi wa umma? Sisi tunasema huwezi kujenga uchumi wa
kipolisi katika mikoa.”
Alisema si watumishi wa umma pekee, bali hata wanasiasa
wakiwamo wabunge na madiwani hawapaswi kuwekwa ndani ovyo, “Ukimaliza kuwaweka
watumishi wa ndani wakaisha, mtaanza kuwekana wenyewe, huoni kuna wabunge wa
CCM nao wanalalamika! Kwa maana watu wa kuweka ndani wameisha mnaanza kuwekana
wenyewe na mwisho wa siku unabaki wewe mwenyewe.”
Alisema katika utumishi kuna eneo la mkuu wa mkoa, wilaya,
mbunge na diwani ambao kwa pamoja wanapaswa kushirikiana ili kufikia azma ya
dira ya Taifa ya maendeleo na vipaumbele vya Rais John Magufuli
Awakuna Polepole na Sugu
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
alipotakiwa kutoa maoni yake juu kauli hiyo ya Mtaka alisema, “Nchi yetu
inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria tuliziojiwekea na huu ndio msimamo wa
CCM na Rais John Magufuli anasimamia hilo.”
Polepole alisema, “Viongozi wanaofanya kazi CCM au
serikalini kwa niaba ya CCM wanapaswa kuheshimu Katiba, sheria na taratibu
nzuri. Wachape kazi zaidi kwa sababu muda haututoshi.”
Akitoa maoni yake, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’ alisema, “Nampongeza sana Mtaka na hao ndio viongozi au
wasaidizi wanaopaswa kumsaidia Rais. Mtaka amekuwa mtu anayeshauri kwani
unapokuwa na viongozi wanaowaweka ndani watumishi wa chini inasababisha kushuka
kwa morali ya kufanya kazi.”</p></div><div><p>Sugu
alisema mtumishi wa umma anapokosea kuna taratibu za kinidhamu na si kuwekwa
ndani jambo ambalo halina tija
“Kama mtu amekosea kwa nini asiwajibishwe kwa sheria za
utumishi? Kwa hiyo alichokisema Mtaka ni kweli kabisa na watendaji wote
mawaziri, wakuu wa mikoa wawe kama Mtaka,” alisema Sugu
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za BInadamu (THDRC),
Onesmo Ole Ngurumwa alisema, “Tunampongeza sana RC Mtaka na wengine wanapaswa
kujitokeza na kukemea vitendo hivi kama alivyofanya Waziri Jafo.”
Alisema matumizi ya kumweka ndani mtu saa 24 au 48,
“Yalilenga kipindi cha ukoloni na kwa mtu anayetishia amani, sasa hivi mtu
anawekwa ndani kwa kuchelewa au kusimamia mradi visivyo jambo ambalo anaweza
kushughulikiwa kwa taratibu za kinidhamu
“Umefika wakati sasa tukaacha tu kusema na tukaenda kubadili
hiyo sheria ambayo imekuwa haitumiki visivyo lakini kwa ma RC na DC wanapaswa
kufuata nyayo za Mtaka ambaye amekuwa RC anayejali na kusimamia misingi ya
utawala bora,” alisema Ole Ngurumwa
Msimamo wa Mtaka wawakuna CCM, Chadema
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 21, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment