Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel
Maganga ameiagiza Idara ya Uhamiaji kuanza msako wa kuwakamata wahamiaji haramu
waliojificha kwenye mashamba na majumbani
Ametoa agizo hilo leo Jumatatu Agosti 6, 2018 wakati
akiwaapisha wakuu wa wilaya ya Kasulu na Buhigwe
Amesema wahamiaji haramu mkoani humo wanatakiwa kukamatwa na
kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili wahukumiwe kifungo
"Watakaobainika kuvunja sheria wafungwe na huko
wakafanye kazi hasa katika kipindi hiki cha kufufua mashamba ya michikichi,
siyo wakakae tu na wakimaliza kifungo warudishwe katika nchi zao," amesema
Ameiomba mahakama kuhakikisha kesi zote za wahamiaji haramu
zinapewa kipaumbele ili kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani, ambao
wanakula chakula bila kuzalisha
Amesema kuna wahamiaji haramu na wakimbizi waliotoroka
kambini wanaishi mitaani na kwenye nyumba za wananchi kinyume cha sheria, jambo
ambalo halikubaliki
"Katika hili hakuna siasa kama kuna kiongozi yeyote wa
kisiasa anawalinda watu hawa ili wampigie kura kipindi cha uchaguzi shauri
yake. Tutasimamia sheria," amesema Maganga
Alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi kwamba si kila mtu
mwenye hati ya kusafiria au kitambulisho cha kupiga kura atapata kitambulisho
cha Taifa
Licha ya matukio ya uhalifu kupungua mkoani Kigoma,
amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha
uhalifu unakoma mkoani humo
RC Kigoma aagiza Idara ya Uhamiaji kuanza msako wa kuwakamata wahamiaji haramu waliojificha
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 06, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment