Uhamiaji wafafanua Watanzania kuzuiwa kuondoka nchini


Idara ya Uhamiaji nchini imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa za Watanzania kuzuiwa kutoka nchini mpaka watakapofuata taratibu za kupata kibali

Kwa mujibu wa idara hiyo taarifa hizo si za kweli zimezushwa na watu kwa nia na madhumuni wanayoyajua wao na kuwa jambo hilo linawahusu wanaofanya kazi zisizo na ujuzi na si raia wengine wanaokwenda nje ya nchi kwa sababu mbalimbali, wamekidhi vigezo vya kisheria

Ufafanuzi huo umetolewa leo jioni Jumatatu Agosti 6, 2018 na msemaji wa idara hiyo, Ally Mtanda

Taarifa hizo zilizosambaa mitandaoni kuanzia juzi zinadai kuwa kwa Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi, wanatakiwa kupeleka mkataba wa kazi katika ofisi za ubalozi ili ugongwe muhuri na kusainiwa

Zinaeleza kuwa mara watakapofika nchini waende Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kupata uthibitisho wa barua kutoka polisi, baadaye kutakiwa kwenda Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) kufanya malipo ya Sh100,000 ili kupata kibali cha kusafiria

Katika ufafanuzi wa idara hiyo leo, mbali na kukanusha umeeleza kuwa Serikali kupitia idara hiyo imeimarisha udhibiti kwa kuwazuia kutoka nchi vijana na wasichana wa Kitanzania wanaokwenda kufanya kazi zisizo za kiujuzi zikiwamo kazi za ndani

Inaeleza kuwa jambo hilo limewafanya wajikute wakiteswa, kunyanyaswa na kufanyishwa kazi zisizo na staha (kutumikishwa kingono) wafikapo katika nchi hizo
Taarifa hiyo imefafanua kuwa utaratibu uliopo sasa kwa kundi hilo ni kuwa, kwa wale ambao wapo nje ya nchi na wana mikataba ya kazi ambayo bado iko hai kwa miezi sita au zaidi, watapaswa kuonyesha nakala za mikataba hiyo na vibali vyao vya kuishi nje ya nchi pindi watakaporejea nchini kwa matembezi na kuahidi kurudi katika nchi zao

“Ifahamike ya kwamba zuio hili haliwahusu raia wengine wanaokwenda nje ya nchi kwa sababu mbalimbali ili mradi wamekidhi vigezo vya kisheria na taratibu za kuondoka nchini,” inaeleza taarifa hiyo

Idara hiyo imetoa onyo kwa wahusika waliotoa taarifa ya uzushi na wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria

“Ifahamike kwamba ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba raia wake wanapokwenda nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali wanakuwa salama na wanafanya kazi zao kwa uhuru bila ya manyanyaso ya aina yoyote,” imesema

Uhamiaji wafafanua Watanzania kuzuiwa kuondoka nchini Uhamiaji wafafanua Watanzania kuzuiwa kuondoka nchini Reviewed by KUSAGANEWS on August 06, 2018 Rating: 5

No comments: