Misa-Tan Yalaani wanahabari Kunyanyaswa.

TAASISI ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (Misa-Tan), imesema inasikitishwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji kwa waandishi wa habari unaoendelea nchini wakati wakitekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma

Aidha, MISA Tanzania inapinga vikali vitendo hivyo viovu na ukandamizwaji wa wanahabari na haki za kupata habari, huku ikiwataka wenye mamlaka kuomba radhi na kuchukua hatua stahiki kwa waliotenda vitendo hivyo vinavyochafua Jeshi la Polisi nchini

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Misa–Tan nakusainiwa na Mwenyekiti wake Salome Kitomari, kwa sasa kuna tishio la unyanyasaji wa waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu kunakofanywa na vyombo vya dola

"Uhuru wa vyombo vya habari ni haki ya msingi inayotamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18, ambayo imetokana na tamko la haki za binadamu la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kupewa nguvu ya kisheria kwa tamko la pamoja la nchi za Afrika ya haki za watu na haki za binadamu," ilisema sehemu ya taarifa hiyo

Alisema MISA Tanzania inasikitishwa na vitendo vya hivi karibuni vya ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji kwa waandishi wa habari unaoendelea nchini wakati wakitekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma

"Tunaungana na wadau wote wa habari na watetezi wa haki za binadamu kupinga vikali vitendo vya kiudhalilishaji kwa mwandishi wa habari za michezo wa Wapo radio, Sillas Mbisse, kwa kupigwa na polisi akiwa chini ya ulinzi wa polisi hao wakati akitekeleza wajibu wake wa kukusanya habari katika Uwanja wa Taifa Agosti 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam,” alisema Kitomari

Alisema, tukio hilo la kufedhehesha na kusikitisha lilitokea Siku ya Simba Day wakati klabu maarufu nchini Simba Sports Club huadhimisha kwa kutambulisha wachezaji na siku hiyo walicheza mchezo wa kirafiki na timu ya Asante Kotoko ya Ghana

Michezo huwakusanya watu pamoja bila kujali rangi zao, itikadi, historia, dini, imani na hadhi ya mtu. Ni maajabu sana kwa mwanahabari kupigwa na polisi mbele ya watu na siyo mashabiki wa timu bali na watu wenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao," Mwenyekiti huyo alisema pia kwa kauli moja, MISA Tanzania inaungana na wadau wengine kupinga kitendo cha kupigwa na kunyanyaswa kwa mwandishi wa habari wa Tanzania Daima, Sitta Tuma, katika kata ya Turwa, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara.

Alisema mwandishi huyo alikamatwa na kisha kupigwa na polisi wakati akikusanya habari za uchaguzi na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi wilayani humo

"Vitendo hivi si tu kwamba vinaondoa uhusiano mzuri wa utendaji kazi kati ya polisi na wanahabari, lakini vinawanyima haki wanahabari kukusanya habari na raia kupewa taarifa iliyokamilika," alibainisha Kitomari

Alisema waandishi wa habari wanafanya kazi ili kuhakikisha kuwa haki hiyo inakuwapo ili kujenga demokrasia na kulinda utawala wa sheria


Misa-Tan Yalaani wanahabari Kunyanyaswa. Misa-Tan Yalaani wanahabari Kunyanyaswa. Reviewed by KUSAGANEWS on August 20, 2018 Rating: 5

No comments: