Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuwasomea maelezo
ya awali viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama
hicho, Freeman Mbowe kutokana na mshtakiwa wa tano, Esther Matiko kushindwa
kufika mahakamani
Akitoa udhuru ya mshtakiwa huyo leo Alhamisi Agosti 2, 2018,
wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala ameieleza mahakama kuwa Matiko
amepigiwa simu ya dharura kutoka katika shule anayosoma mwanaye mjini
Nairobi, Kenya na kulazimika kwenda
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alimuhoji mdhamini
wa mbunge huyo wa Tarime Mjini juu ya sababu za kwenda Nairobi na kujibiwa kuwa
hata yeye hafahamu zaidi ya kuelezwa na Matiko kuwa anakwenda shule
anayosoma mwanaye
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali mkuu,
Faraja Nchimbi umemlaumu mdhamini huyo kwa kutojua sababu ya
kilichompeleka mbunge huyo Nairobi, kutaka akirejea awe na uthibitisho
"Upande wa mashtaka hatuna la kufanya ila kesi
itakapotajwa inabidi aieleze mahakama pamoja na udhibitisho wa nini alichoitiwa
huko" amesema Nchimbi
Nchimbi aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti
6, 2018 huku Kibatala akiomba ipangiwe Agosti, 13, 2018 kwa kuwa Agosti 6
atakuwa na kesi Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Mashauri alikubaliana na ombi la upande wa
Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6
Hakimu Mashauri pia aliwaonya wanaompigia simu, bila
kuwataja majina amesema akiwa kazini anakuwa hakimu na akiwa nyumbani anakuwa
Mashauri
“Nikiwa nyumbani ni Mashauri na nikiwa kazini ni Hakimu
hivyo wanaonipigia simu nikiwa nyumbani huo sio utaratibu,” amesema
hakimu Mashauri
Mbali na Mbowe washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni naibu
makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); mbunge wa
Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa
Wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji;
mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Musoma Vijijini, John Heche; mbunge wa
Bunda, Ester Bulaya na Matiko
Mbowe na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwamo
kuchochea ghasia, kukaidi amri ya polisi, uchochezi na uasi
Wanadaiwa kufanya makosa hayo, Februari 16 wakati polisi
wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana.
Katika tukio hilo,
mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),
Akwilina Akwilini alipigwa risasi akiwa kwenye daladala, eneo la Kinondoni,
Mkwajuni
Matiko akwamisha kesi ya vigogo Chadema
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 02, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 02, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment