Mamba wasababisha vifo vya watu zaidi ya 50


WANANCHI wa vijiji vilivyopo kata ya Udinde na Kapalala, tarafa ya Kwimba wilayani Songwe, wameiomba serikali kuwajengea kivuko cha muda kunusuru vifo vitokanavyo na kuliwa na mamba wanapovuka Mto Kikamba.

Mto huo unaounganisha vijiji vya kata za Kapalala na Udinde, umesababisha vifo vya watu zaidi ya 50 wakiwamo wazazi wa mbunge wa jimbo hilo kuliwa na mamba hao

Stella Philimon, mkazi wa kijiji cha Rukwa, alisema chanzo cha watu kuliwa ama kujeruhiwa na mamba ni kutokana na kukosekana kwa daraja la kuvuka wanapokwenda kuchota maji katika mto huo au kuvuka kwenda kutafuta huduma za kijamii upande wa pili

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Udinde, Oscar Leonard alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa mwaka 1991, wazazi wa Mbunge wa Jimbo hilo Phillipo Mulugo, waliliwa na mamba wakati wakichota maji. Alisema mama yake aliuawa katika mto huo na baba aliuawa Ziwa Rukwa, hali iliyozua taharuki

Alisema zaidi ya watu 50 waliliwa na mamba katika mto Kikamba na wengine pembezoni mwa Ziwa Rukwa, huku 15 wakiachwa na vilema vya maisha

Kutokana na hali hiyo, Leonard kupitia mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge Mulugo, alisema hoja za wananchi zina ukweli na kueleza kuwa kujengwa kwa daraja ndiyo suluhisho la tatizo hilo

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Abraham Sambila, alisema maisha ya wananchi wa eneo hilo ni ya wasiwasi kufuatia uwepo wa mamba katika mto huo na Ziwa Rukwa, hasa kipindi cha mvua za masika

Alisema watakapo kaa vikao na kujadili tatizo hilo watawatuma mainjinia kufanya tathmini ya gharama ya ujenzi na kuomba fedha serikalini katika bajeti ya mwakani ili kujenga daraja na kumaliza tatizo hilo

Naye Mbunge wa Songwe Mulugo, aliwaambia wananchi hao kuwa anapokumbuka wazazi wake walivyofariki kwa kuliwa na mamba baadhi ya viungo vyao, mwili wake unatetemeka na kukosa raha

Alisema sababu kubwa ilikuwa ni uhaba wa maji na miundombinu ya barabara na madaraja

Alisema ombi la wananchi hao atalipeleka kwenye vikao vya Bunge, ili kuliombea fedha kwa kuwa alisema serikali ni sikivu na anaamini italifanyia kazi

Kuhusu maji, Mulugo alisema ilikuwa ni kero kubwa, lakini serikali imewapatia Sh. bilioni 1.2 kwa ajili ya kusambaza miradi saba ya maji na ujenzi utakamilika baada ya miezi sita

Mulugo alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangala, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo hivi karibuni, alisikia kilio cha wananchi kuhusu mamba hao ambao wanaongezeka siku hadi siku na kuziagiza mamlaka husika kufanya utaratibu wa kuvuna mamba hao

Mamba wasababisha vifo vya watu zaidi ya 50 Mamba wasababisha vifo vya watu zaidi ya 50 Reviewed by KUSAGANEWS on August 21, 2018 Rating: 5

No comments: