Makonda Kuja na Mkakati wa Kuthibiti Wezi na Matapeli


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mfumo wa anwani za makazi na mwongozo wa postikodi ukikamilika utasaidia kudhibiti wezi na matapeli katika Jiji la Dar es Salaam

Amesema pia utarahisisha huduma na kumwezesha kila mwananchi kuwa na anwani, kuwasaidia wageni kujua maeneo, kulisaidia Jeshi la Zimamoto na Ukoaji kufika haraka kwenye eneo lenye tukio

Aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa warsha kwa viongozi wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam iliyohusu ukusanyaji wa taarifa za anwani za makazi na wanakaya, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA

"Mfumo huu ni ukombozi kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa utarahisisha huduma na kuwezesha kila mwananchi kuwa na anwani

"Pia utasaidia Jiji la Dar es Salaam kuwa katika mpangilio wa kisasa na kuhakikisha mitaa yote inawekwa katika mfumo wa anwani za makazi na postikodi," alisema Makonda

Alieleza kuwa mfumo huo utasaidia kuwaunganisha wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa utakuwa katika mpangilio wa kisasa

Alisema mpango huo utawasaidia wageni wanaoingia katika jiji hilo kutokutapeliwa wanapotumia vyombo vya usafiri kufika maeneo wanayokwenda

"Abiria mgeni akishuka uwanja wa ndege au kituo cha mabasi cha Ubungo itakuwa rahisi kwake kutoa kiwango sahihi cha pesa huko aendako kwa sababu atakuwa anafahamu umbali na sehemu aendako," alisema Makonda

Aidha, aliwaomba TCRA kupeleka elimu hiyo kwa madiwani na wenyeviti wa mitaa ili kuwajengea uelewa

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Connie Francis, alisema utaratibu wa kukusanya taarifa za anwani za makazi umeboreshwa na kwa sasa taarifa hizo zitachukuliwa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki(e-PRS

Alisema mfumo huo utasaidia wananchi kujitambulisha anapoishi na kupatiwa huduma kwa urahisi, kuboresha huduma za uokoaji na za dharura, kurahisisha huduma za misaada inapotokea maafa, kufikisha mizigo nyumbani na ofisini

"TCRA inatambua kuwa jukumu la kutoa majina ya mitaa na barabara na kuweka namba za nyumba kisheria ni la mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini kwa kuzingatia umuhimu wa kuboresha utoaji na ufikishaji wa huduma za mawasiliano kwa jamii, TCRA ilisimamia utekelezaji wa mpango huu katika awamu ya majaribio," alisema Francis

Alisema utekelezaji wa awali ulifanyika katika baadhi ya kata za majiji zikiwamo kata nane za Jiji la Arusha, nane za Jiji la Dodoma na 45 kwa Jiji la Dar es Salaam, ambalo umefanyika kwa awamu tatu; ya kwanza zilikuwa kata 32, awamu ya pili 13 na awamu ya tatu utekelezaji wake unakamilishwa hivi karibuni

Makonda Kuja na Mkakati wa Kuthibiti Wezi na Matapeli Makonda Kuja na Mkakati wa Kuthibiti Wezi na Matapeli Reviewed by KUSAGANEWS on August 20, 2018 Rating: 5

No comments: