Madc waonywa Kutumia Vibaya Madaraka Yao

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo amewataka Wakuu wapya wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni kuacha tabia ya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo na kuwaweka rumande wananchi pamoja na watumishi wa umma hali inayopelekea kuichukia serikali yao.

Mhe. Jafo aliyasema hayo leo Jijini Dodoma kwenye kikao kazi na Wakuu hao wa wilaya kwa lengo la kuwapa maelekezo ya kazi ambapo mada kuu ya kikao hicho ni mahusiano na mawasiliano kazini pamoja na kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo

“Msiende kuwa vyanzo vya migogoro kwenye Wilaya zenu, tumekuwa tukishuhudia migogoro baina ya Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala pamoja na Wabunge, hatuwezi kwenda hivi, katengenezeni serikali” Alisema Waziri Jafo

Aidha aliwataka Wakuu hao wapya wa Wilaya kutoa ushirikiano kwa wale wanaotekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na siyo vinginevyo ikiwa ni pamoja kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya afya na elimu unaoendelea kote nchini

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Injinia Mussa Iyombe amewataka Wakuu hao wa wilaya kuzitendea haki nafasi walizopewa kwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo hasa pale wanapomuadhibu mtumishi aliyekosea. 

“Serikali ina taratibu zake, baadhi ya wakuu wa wilaya walikuwa wanatia aibu, kama kuna mtumishi kakosea, tumia mamlaka zinazomuongoza kumshughulikia, na sio kusimamisha watu kazi hovyo, kutumbua tumbua hovyo” Alisisitiza Injinia Iyombe
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amesema watahakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia kasi ya Rais Dkt John Pombe Magufuli

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amesema ni muda wa kufanya kazi na sio kuongea ongea sana huku akiahidi kufuata miongozo iliyotolewa na viongozi wa juu kwenye utekelezaji wa majukumu yake


Madc waonywa Kutumia Vibaya Madaraka Yao Madc waonywa Kutumia Vibaya Madaraka Yao Reviewed by KUSAGANEWS on August 15, 2018 Rating: 5

No comments: