Lukuvi akabidhiwa kero za ardhi Tabora


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi atakwenda katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kutatua kero kubwa za ardhi. 

Pia, Majaliwa amezitaka wilaya zote kuhakikisha zinakuwa na shule moja ya kidato cha tano na sita kila tarafa nchini na Serikali itapeleka walimu. 

Ameyasema hayo jana jioni Agosti 18, 2018 wakati akizungumza na wananchi wa manispaa hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Chipukizi. 

Majaliwa aliyasema hayo baada ya wabunge na wananchi kueleza changamoto kubwa zinazowakabili ikiwamo ya migogoro ya ardhi iliyodumu muda mrefu. 

“Waziri wa Ardhi atakuja hapa na ramani zake, atakutana na watendaji na kumaliza matatizo yote makubwa ya ardhi na yale madogo madogo yatashughulikiwa na mkuu wa wilaya,” amesema Majaliwa. 

Kuhusu ujenzi wa shule, Majaliwa amesema uwapo wa shule hizo utaamsha ari ya wanafunzi kusoma kwa bidii, jambo litakaloongeza idadi ya wanaoendelea na masomo ya kidato cha tano na sita. 

Pia, Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wote kuanzia halmashauri hadi vijiji wawasimamie wanafunzi wa kike na wahakikishe wanamaliza masomo bila ya kukatishwa. 

“Huu ni mkakati wa taifa tunataka watoto wa kike wote walindwe ili waweze kumaliza shule na marufuku kukatisha elimu yao, iwe kwa kuwapa ujauzito au kuwaoa, adhabu yake ni kali,” amesema. 

Majaliwa jana jioni alimaliza ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora baada ya kufanya ziara wilaya za Igunga, Nzega na Manispaa ya Tabora

Lukuvi akabidhiwa kero za ardhi Tabora Lukuvi akabidhiwa kero za ardhi Tabora Reviewed by KUSAGANEWS on August 19, 2018 Rating: 5

No comments: