Lugola azibana kampuni, ataka zirejeshe Sh28.5 bilioni


Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola ametoa siku 15 kwa kampuni saba zilizobainika kufanya ufisadi katika mradi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kurejesha Sh28.5bilioni walizolipwa

Amezitaka kampuni hizo kutekeleza agizo hilo ili kuepuka kuwa wateja wa mahakama ya mafisadi

Ufisadi huo uligundulika katika ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Februari, 2016

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 4, mjini Dodoma ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na wamiliki wa kampuni hizo kuomba wawasilisha vielelezo vya malipo hayo

Lugola amezitaja kampuni hizo na kiasi cha fedha katika mabano kuwa ni Gotham International Ltd (Sh2.8 bilioni), Iris Corporation Berhard (Sh22.9 bilioni), Gwiholoto impex Ltd (Sh 946.4 milioni

Nyingine ni Skyes Travel Agent (Sh6 milioni), Dk Shija Paulo Rimoy (Sh27 milioni), Aste Insurance (Sh1.2 bilioni) na BMTL (Sh 569.1 milioni) ambayo imekubali kurejesha fedha hizo

Lugola amesema wamiliki hao na watu wengine wanaopata zabuni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Serikali wanatakiwa kutofanya  ufisadi kupitia kivuli cha mikataba

“Ninawaomba msicheze na Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu imeapa kulinda rasilimali za Watanzania. Kuna mahakama ya mafisadi,” amesema

“Takwimu nilizonazo  mahakama ile bado ina uhaba wa mafisadi, mimi nina dhamana ya kuitafutia wateja. Nyinyi tuliohojiana leo muombe msiwe miongoni mwa wateja ninaoitafutia mahakama hiyo.”

Kuhusu hatima ya aliyekuwa mkurugenzi wa Nida, Dickson Maimu na kampuni ya Iris Corporation Berhard ya nchini Malasia ambayo ililipwa Sh32 bilioni na Nida kwa ajili ya kuleta mtambo wa kutengenezea kadi ghafi nchini,  amesema itajulikana Agosti 17, 2018

“Maimu yeye ametusaidia kupata maelezo ya ziada kuhusu ile kampuni, baada ya siku 14 watakavyokuja ndio tutajua hatima yake, tutajua kama suala litaisha ama la,” amesema Lugola

Amesema Maimu na mmiliki wa kampuni ya Jack Ghotham waliitika wito wake jana na kutoa maelezo ya ziada ambayo yatawasaidia katika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo

Julai 25, 2018 Lugola aliipa wiki mbili kampuni ya Iris na Ghotham kwenda ofisini kwake kujadiliana jinsi ya kumaliza suala hilo
Lugola azibana kampuni, ataka zirejeshe Sh28.5 bilioni Lugola azibana kampuni, ataka zirejeshe Sh28.5 bilioni Reviewed by KUSAGANEWS on August 04, 2018 Rating: 5

No comments: