Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward
Lowassa amemjia juu mbunge wa zamani wa Monduli, Julius Kalanga akidai kwamba
amesema, “Nimemtanguliza Ikulu.”
Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Monduli hadi mwaka 2015
alipojiunga na Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama
hicho akiungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, alisema pia kwamba kuna madai
yanayosambaa kwamba yupo mbioni kuwatoa wabunge na madiwani wa Chadema na
kuwapeleka CCM
“Wanasema kazi hiyo nimeivalia njuga na ninaifanya vizuri
sana na kwamba tumekubaliana na Rais (John) Magufuli nimfanyie kazi hii. Waongo
wakubwa hao, tena wamesema Mto wa Mbu, wamesema Monduli na kwenye magazeti
kadhaa na kwenye mablog lakini nataka niwaeleze kwamba ni waongo wakubwa hao,”
alisema waziri mkuu huyo wa zamani huko Migungani, Arusha hivi karibuni
Alisema, “Kwa hiyo nimesimama kusema sijamtuma mtu yeyote
kwa Rais na sina mpango wa kufanya hivyo, acheni kumsingizia Rais acheni kunisingizia
ugomvi kati ya Rais na mimi, sina ugomvi na Rais Magufuli.”
Aidha, Lowassa alisisitiza, “Kuna mashindano ya kuhama
vyama, wanafanya nchi nzima, wanaohama nawatakia kila la heri. Lakini
wasitafute mchawi, waseme naenda kwa hoja zangu hizi hizi, sio kwa sababu
fulani amenitanguliza.”
“Aliyekuwa mbunge wa Monduli (Julius Kalanga) alisema
hadharani amenitanguliza Ikulu, huo ni uongo wa kutupwa… kwa hiyo mimi sina
miguu? Kama nataka kwenda si nitakwenda kwa miguu yangu, eti anasema nimemtuma
nimemtanguliza kwenda Ikulu, watu wa Monduli wote watahamia chama chake
“Anasema uongo kwenye kinywa chake, lakini nasema huhitaji
kuomba ruhusa kuhama chama, hiari yako mwenyewe.”
Hata hivyo, jana alipoulizwa kuhusu madai hayo, Kalanga
ambaye baada ya kuhamia CCM ameteuliwa na chama hicho kuwania tena nafasi hiyo
amekanusha kusema hayo akisisitiza kwamba hajawasiliana na Lowassa kwa muda
mrefu
Kuhusu wanasiasa kuhama vyama, Lowassa ambaye pia ni mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema alisema, “Ndugu zangu wala msitishike, kuhama vyama ni
utaratibu wa kisiasa ndiyo mchezo wa wanasiasa. Raila Odinga amehama vyama mara
saba.”
Alitoa mfano wa Nigeria akisema kuelekea uchaguzi mkuu wa
nchi hiyo, tayari kuna wanasiasa karibu 400 kwenye Bunge kubwa la nchi hiyo na
zaidi ya 200 kwa Bunge la kawaida ambao wamehamia vyama vingine
“Wanahama usiku na mchana, ukisikia mtu anahama funika
blanketi lako... ana hoja zake na sababu zake na nyingi ni za uongo. Zile za
kweli utakutana na wenzako mbele ya safari. Sasa usisingizie watu. Amesingizia
mbunge wa Monduli kwamba anakwenda kwa sababu hakuna maendeleo anayoweza
kufanya, mwongo.”
“Nimekaa Monduli miaka tuliyokaa tumefanya maendeleo,
hatukufanya? Akajibiwa na wananchi, “tumefanyaaaa.” Akaendelea, “Tuna shule ya
sekondari katika kila kata, tunazo hatunazo?” Akajibiwa, “Tunazoooo.”
Akaendelea kuhoji, “Tunayo hospitali ya wilaya, tunayo hatunayo? Akajibiwa,
“Tunayoooo.” Mwisho akauliza, “Tuna barabara ya lami, tunayo hatunayo?
Akaambiwa “Tunayoooo”. Kisha akahoji, “Mungu atupe nini?”
Kalanga aruka Licha ya kukanusha kutoa maneno hayo, Kalanga
alisema, “Nina miezi zaidi ya sita sijaonana na Lowassa. Hizi taarifa ambazo
nimemsikia akinituhumu Mzee Lowassa nadhani watu wake wamempotosha.”
Kalanga alisema anamheshimu Lowassa na asingependa malumbano
naye.
Kabla ya kujiunga na
Chadema mwaka 2015, Kalanga alikuwa diwani wa Lepurko na mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM), Wilaya ya Monduli, huku Lowassa akiwa mbunge wake
Lowassa acharuka kuhusishwa na wabunge wanaohamia CCM
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 15, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment