Kauli ya mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kwamba mtu
akihama chama ahame na uwakilishi wake imeibua tena hoja ya kuwapo mgombea
binafsi
Mwaka 1993, Mchungaji Christopher Mtikila alifungua kesi ya
kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kahwa
Lugakingira akitaka kutambuliwa kwa mgombea binafsi
Jaji Lugakingira ambaye kama ilivyo kwa Mchungaji Mtikila
wote ni marehemu, alikubaliana na hoja kwamba kugombea kama mtu binafsi ni haki
ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya haki ya kuchagua viongozi na
haki ya kugombea uongozi
Hata hivyo, mwaka 1994 hoja hiyo ilikwama bungeni baada ya
chombo hicho kufanya mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 kwa kuzuia
wagombea binafsi
Mwaka 2005, Mchungaji Mtikila alifungua tena kesi Mahakama
Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba na jopo la
majaji watatu, chini ya Amiri Manento (akiwa Jaji Kiongozi) lilikubaliana na
hoja za mlalamikaji na kuruhusu mgombea binafsi.
Lakini mwaka 2010, Serikali ilikata rufaa Mahakama ya Rufaa
ambako majaji saba chini Jaji Mkuu wakati huo, Augustino Ramadhani walisema
hakuna mahakama yoyote nchini yenye uwezo wa kisheria kusikiliza kesi inayotaka
mgombea binafsi na kwamba mahakama za chini zilijipachika madaraka ya kibunge
ya kutunga sheria badala ya kuzitafsiri
Jana, wanasiasa na wasomi waliozungumza na Mwananchi kuhusu
kauli ya Nape waliibua hoja ya mgombea binafsi wakisema wagombea watakuwa huru
pasipo kikwazo
Agosti 16, Nape akizungumza wakati wa mafunzo ya siku mbili
ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge na wajumbe wa Tume ya
Utumishi wa Bunge, alisema ifike mahali iruhusiwe mtu akihama chama ahame na
ubunge au cheo alichonacho
Akizungumzia kauli ya Nape, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa wa CCM, Ngemela Lubinga alisema haiwezekani kwa sababu uwakilishi ni
mali ya chama na si mtu
Huku akimtaka Nape kuweka wazi kama ana ajenda nyingine ya
siri ili ifahamike, Lubinga alisema haiwezekani hata kubadilisha sheria kwa
sababu suala hilo lina mkanganyiko
Alisema itikadi ya chama ndiyo inakifanya kishinde uchaguzi,
hivyo kuhama na uwakilishi ni kuwanyima haki wapigakura waliomchagua kwa itikadi
ya chama chake
Alisema ubunge au udiwani ni mali ya chama, hivyo mtu hawezi
kuhama na wadhifa wake kwa sababu si mali ya chama anachohamia
“Jambo hili linaeleweka, halihitaji staretegic analysis
(uchambuzi wa kimkakati). Atuambie kama ana ajenda ya siri,” alisema Lubinga
Akiwa na mtazamo kama huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (Out), Hamad Salim alisema kuhalalisha wabunge au madiwani kuhama na
vyama na vyeo vyao kutaondoa nguvu ya wananchi kuchagua viongozi na kwamba
wanasiasa wataendelea kufanya mchezo huo kila wanapojisikia
“Nadhani utaratibu uliopo unafaa na unakidhi matakwa.
Tuangalie vyanzo vingine vya hawa wanaohama ni nini. Pia, tunaweza kujadili
mahitaji ya kuwa na wagombea binafsi,” alisema Salim
Hata hivyo, aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa
Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema kuna umuhimu wa kuruhusu wagombea
binafsi ili watakaohamia chama kingine wahame na nafasi zao,
“Kikatiba na kisheria hili haliwezekani, lakini tungekuwa na
watu independent (huru), ingewezekana. Lazima element ya kuchaguliwa iwepo
ndipo mtu awe mbunge au diwani na si kuhama tu.”
Akiwa na mtazamo kama huo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alisema sasa ni wakati wa kuruhusu
wagombea binafsi kwa sababu kuna watu ambao wako kwenye vyama kwa sababu ya
kutimiza matakwa ya kisheria lakini mioyo yao haipo huko
Alisema hoja ya muhimu kwa sasa si kuhama na ubunge, bali
kujiuliza ni kwa nini watu hao wanahama kutoka chama kimoja kwenda kingine na
kupewa nafasi tena ya kugombea huko
“Lazima turuhusu mgombea huru, kuna watu wana ushawishi na
wangependa kujidhamini wenyewe lakini kwa sababu ya matakwa ya kisheria
wanalazimika kujiunga na vyama vya siasa.”
Dk Bana alisema baadhi ya wabunge hao ndio wanaovihama vyama
vyao wakihofia hatima yao ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020
Alisema wanasiasa wanapima upepo na kuamua kuvihama vyama
vyao ili kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi ujao
Kauli ya Nape yaibua upya hoja ya mgombea binafsi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 20, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment