Kauli ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,
Atashasta Nditiye kuhusu udhibiti wa umiliki wa zaidi ya laini moja ya simu
imezua mjadala huku watu wengi wakionyesha kutoelewa dhamira ya Serikali katika
suala hilo
Mjadala huo ulionekana kushika kasi mitandaoni watu wakihoji
sababu za Serikali kufikia uamuzi huo, huku wengine wakitaka kujua hatima ya
wanaomiliki laini zaidi ya moja
Juzi, Nditiye aliripotiwa na kituo kimoja cha televisheni
akieleza kuwa Serikali itaanza kudhibiti umiliki holela wa laini za simu kwa
kutumia alama za vidole katika usajili, hivyo mtu atakayehitaji laini zaidi ya
moja atalazimika kujazwa fomu ya kueleza kwa nini apatiwe
Kwa mujibu wa Nditiye, katika kufanikisha udhibiti huo
vitatumika vitambulisho vilivyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(Nida).
Utaratibu huo mpya utamtaka anayetaka kusajili laini zaidi
ya moja atambuliwe na kampuni za simu na kujua kuwa tayari ana laini ya kwanza,
hivyo lazima atajaza fomu maalumu kueleza kwa nini anataka ile ya pili
Sambamba na hilo, Nditiye alisema kabla ya mwaka huu kuisha
laini za simu zitaanza kuuzwa kwenye maduka rasmi na mtu anayesajili
atachukuliwa alama za vidole na picha yake
Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa wizara hiyo, Isack
Kamwele alithibitisha kuwepo kwa mpango huo ambao utaanza kwa Serikali kukaa na
wataalamu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), kuangalia uwezekano wa kuwa na
kanuni au sheria za kusimamia hilo. Alisema uamuzi wa kuelekeza matumizi ya
laini moja ya simu unalenga kukabiliana na wizi na utapeli ambao umekuwa
ukifanywa kwa njia ya simu
“Baada ya kulivalia njuga suala la utapeli kwa njia ya simu,
wale watu wanaotuma meseji ya kuelekeza watumiwe pesa walikamatwa na wengine
wana laini zaidi ya 10, mwingine 30 sasa hii ni hatari,” alisema Kamwele
Alisema baada ya utaratibu huo kupitishwa mtu mmoja atakuwa
na namba ya simu kutoka mtandao mmoja na akiweza kuthibitisha matumizi ya namba
ya simu ya mtandao mwingine ndipo atakapopewa
Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala alipotakiwa kuzungumzia
suala hilo alisema hajasikia na hivyo akataka atafutwe naibu waziri
aliyelizungumzia
Maoni ya wananchi
Albert Ryeyamamu, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam,
alisema utaratibu huo utawabana watumiaji wa simu ambao wakati mwingine
wanamiliki laini zaidi ya moja kutokana na umuhimu wa matumizi kulingana na
mitandao husika
‘Mfano mimi nina laini ya mawasiliano na nyingine naitumia
kwa ajili ya intaneti, hiyo ni kutokana na unafuu wa gharama ninaoupata. Sasa
unaponilazimisha niwe na namba moja itanipa wakati mgumu,” alisema
Naye Rehema Grey mkazi wa Kinondoni aliishauri Serikali
kuangalia upya kabla ya kuanza utelekezaji wa mpango huo kwa kuwa unaweza
kuharibu biashara kwa kampuni za simu na kuwabana watumiaji
“Sioni kama ni sawa kwani huku ni kuingilia uhuru wa
mawasiliano na athari yake haitakuwa kwa watumiaji tu, bali hata kampuni za
simu zitakosa wateja kwa sababu watu tuna simu za laini mbili na matumizi yangu
mfano hayawezi kufaa kwa namba moja pekee,” alisema
Kampuni zajipanga
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mawasiliano wa Halotel,
Mhina Semwenda alisema hawajapata taarifa hiyo rasmi kwa kuwa yanapotokea
mabadiliko kampuni za simu hupewa mwongozo. “Sisi wenyewe tumeona na kusikia
kwenye mitandao, hatujapata taarifa rasmi kutoka kwa waziri mwenye mamlaka ya
mawasiliano, hivyo siwezi kusema utaathiri au kuleta faida zipi,” alisema
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Airtel, Jackson Mbando
alisema taarifa hiyo wameipata kwenye vyombo vya habari na mitandaoni, lakini
watakapoipata rasmi wataizungumzia
Juhudi za kuwapata wasemaji wa kampuni zingine za
mawasiliano hazikuzaa matunda
Kauli ya naibu waziri juu ya laini za simu yazua mazito
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 18, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment