Kauli ya IGP Sirro Kuhusu Kupigwa Mwanahabari Yaanza Kutibua Mapya


Wadau wa masuala ya habari na wanasheria wamepinga kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kwamba mwanahabari Silas Mbise alishambuliwa na polisi kwa kutotii sheria

Sirro aliyasema hayo jana jijini Arusha wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuulizwa juu ya hatua za uchunguzi wa jalada lililofunguliwa polisi la kupigwa kwa mwandishi huyo wa Wapo Redio katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Agosti 8

“Taarifa za awali tulizonazo ni kwamba mwandishi huyo alikuwa mbishi katika kutii agizo la askari aliyemkataza kuingia sehemu ambayo walizuiliwa hadi kufikia kumkaba askari akilazimisha kuingia ndipo askari naye akapata hasira wakafikia hali hiyo,” alisema IGP Sirro akizungumzia tukio hilo lililotokea siku maalumu ya Klabu ya Simba (Simba Day)

Alisema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na baadaye polisi itaeleza ukweli na hatua za kisheria zitafuata dhidi ya atakayebainika kutenda kosa

“Ngoja tuone upelelezi na ushahidi utasemaje, ukimalizika na kama kuna aliyemuonea mwenzake hatua za kisheria zitafuata hivyo kama askari alimpiga kwa kumuonea atachukuliwa hatua za kisheria na kama mwandishi naye alifanya fujo huko na kukimbilia kwenye kamera aonekane tutamchukulia hatua pia maana hakuna aliye juu ya sheria,” alisema

Sirro pia alitumia nafasi hiyo kuwataka waandishi kufanya kazi zao vyema kwa kutii mamlaka na sheria zilizopo ili kufanya kazi zao kwa weledi

Agosti 9, ikiwa ni siku moja baada ya Mbise kupigwa, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema IGP Sirro ameagiza kufunguliwa kwa majalada mawili, likiwemo la malalamiko ya Mbise ya kupigwa na la kuangalia maelezo ya polisi kuwa Mbise hakutii sheria.

 Baada ya kauli ya Sirro jana, wadau wa habari na wanasheria walisema mkuu huyo wa polisi ametoa hukumu wakati bado uchunguzi wa suala hilo haujakamilika

Walisema kauli yake haiwezi kutoa haki kwa mwandishi wa habari aliyepigwa

Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (Tef), Jesse Kwayu alisema video zilizorekodiwa zinaonyesha mwandishi akipigwa na polisi akiwa hana silaha, amelala chini na kuinua mikono juu

Alisema huo ni mfululizo wa matukio ya jeshi hilo kuwanyanyasa raia

“Kauli ya IGP ni ya kusikitisha, its unfortunate statement (ni kauli ya kusikitisha). Asimamie sheria na weledi wa polisi katika kutekeleza majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema Kwayu

Pia alihoji ni sehemu gani ambayo mwandishi wa habari haruhusiwi kuingia akiwa katika uwanja huo kama IGP Sirro alivyoeleza

Alisema mkuu huyo wa polisi anajaribu kufukia maovu ya jeshi hilo badala ya kukemea

Akiwa na mtazamo kama huo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alipendekeza kuwepo chombo kitakachosimamia malalamiko yote dhidi ya Jeshi la Polisi

Olengurumwa alisema alitarajia kusikia IGP akikemea suala hilo kama walivyofanya mawaziri, lakini ameanza kuwakingia kifua askari waliohusika kwenye unyanyasaji huo kabla hata uchunguzi haujakamilika

“Kitendo cha yeye kutoa tamko kabla hata uchunguzi haujakamilika inaonyesha dhamira yake ya kutaka kuwalinda askari wake. Ifike mahali tuwe na chombo huru ambacho kitasimamia malalamiko ya matukio ambayo Jeshi la Polisi linahusika,” alisema

Mwanasheria na Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), John Seka alisema kauli ya mkuu wa polisi inawaaminisha watu kwamba askari hawakufanya kosa kumshambulia mwandishi huyo

Alisema video inaonyesha askari wakimshambulia raia ambaye alikuwa haonyeshi upinzani wowote

Seka alisema kuwa hata kama mwandishi huyo alileta upinzani, ilifikia hatua akasalimu amri kama ilivyoonekana, lakini bado waliendelea kumpiga. “Kuna haja ya askari wetu kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi yao. Msimamizi wa mkuu wa taratibu hizo ni IGP Sirro, ninatumaini watatenda haki kwa mwandishi wa habari,” alisema

Kauli ya IGP Sirro Kuhusu Kupigwa Mwanahabari Yaanza Kutibua Mapya Kauli ya IGP Sirro Kuhusu Kupigwa Mwanahabari Yaanza Kutibua Mapya Reviewed by KUSAGANEWS on August 17, 2018 Rating: 5

No comments: