Dar es Salaam. Fred, mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, ameelezea kilichotokea Monduli katika mchakato wa kumpata mgombea
ubunge wa jimbo hilo akisema, “Sikuwahi kuchukua fomu na ninaiheshimu sana
Chadema.”
Fred ametoa kauli hiyo kipindi ambacho jina lake limekuwa
kwenye mijadala ndani na nje ya Chadema kwamba, alijitokeza kuchukua fomu ya
kuwania ubunge wa jimbo hilo lililoongozwa na baba yake (Lowassa) kwa miaka 20
Lowassa alikuwa mbunge wa Monduli kati ya 1995-2015.
Uchaguzi wa ubunge katika majimbo matatu likiwamo la Monduli na udiwani wa kata
21 utafanyika Septemba 16, baada ya wabunge wawili kuhama Chadema na kwenda CCM
huku aliyekuwa mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani ‘Profesa
Majimarefu’ akifariki dunia Julai 2
Waliotimkia CCM ni Mwita Waitara (Ukonga) na Julius Kalanga
(Monduli) ambao Kamati Kuu ya CCM imewapitisha kugombea tena ubunge pamoja na
Timotheo Mzava anayewania Korogwe Vijijini
Wakati CCM ikiwapata wagombea kwenye majimbo hayo, Chadema
imewapitisha Asia Msangi (Ukonga) na Amina Saguti kuwania Korogwe Vijijini,
huku Monduli akiwa ni Yonas Laizer ambapo kampeni za uchaguzi huo zinaanza
Agosti 21
Jana, Mwananchi lilizungumza na Fred kujua kilichojiri hadi
kujitoa kwake ambapo alisema, “Nawaheshimu sana sana Chadema, walitupa heshima
kubwa sana mwaka 2015 kwa mzee (Lowassa) kuwa mgombea na wana CCM waliojiunga
na mabadiliko nao kupewa fursa ya kugombea.”
Katika uchaguzi wa mwaka huo, Lowassa na Ukawa walitoa
changamoto kwa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli, ambapo mgombea huyo wa Ukawa
alipata kura 6,072,848, huku Dk Magufuli akitagazwa mshindi kwa kupata kura
8,882,935
Fred ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya watano wa Lowassa na
mkewe, Regina alipoulizwa kama fomu alichukua ya kugombea Monduli, alisema,
“Fomu sijawahi kuchukua (ingawa) nia ya kutaka kushiriki uongozi Monduli ninayo
lakini si sasa.”
Alikiri kuwapo kwa ushawishi kutoka kwa wanachama wa Chadema
lakini aliona siyo wakati wake
Alisema yeye na familia watamuunga mkono mgombea mwenye
nguvu ya mabadiliko atakayepitishwa
“(Lakini) alichofanya ndugu yetu Kalanga, amekosa fadhila
kwa wana Monduli, nasikitika tunaingia katika uchaguzi mdogo kwa mtu aliyekosa
fadhira.”
Fred alisema Monduli inatizamwa kwa jicho la kipekee
kutokana na kuwa na wilaya iliyotoa mawaziri wakuu wawili ambao ni Lowassa na
Hayati Edward Sokoine ambao makazi yao hayaachani hata kilomita mbili
“Mgombea wa ‘spirit’ (nguvu) ya mabadiliko nitamuunga
mkono,” alisema Fred huku akisisitiza kwamba familia ya Lowassa itaendelea
kutoa huduma kwa wana Monduli. “Familia ya Lowassa siku zote itaendelea kuwa
watumishi kwa jamii ya Monduli bila cheo chochote.”
Alipoulizwa juu ya mtazamo wake wa chaguzi za hivi karibuni,
Fred alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inapaswa kuyafanyia kazi
malalamiko yanayotolewa
“Nchi kubwa kama Marekani wanaongea, (hivyo) kuna jambo la
kutafakari kwa nini wameongea,” alisema Fred akizungumzia kauli iliyotolewa na
Ubalozi wa Marekani nchini. Nakubaliana na (Kabwe) Zitto (kiongozi wa
ACT-Wazalendo) kwamba ni muda muafaka kufanya mkutano wa kitaifa wa maridhiano
ya kisiasa.”
Hivi karibuni, Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini
alisema kutokana na hali ilivyo nchini, umefika wakati ufanyike mkutano wa
maridhiano ya kisiasa ili kurejesha kuaminiana na kusonga mbele kama Taifa
Fred Lowassa azungumzia kilichotokea Monduli, ataka maridhiano kitaifa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 18, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment