Chadema waelezea kilichowanyima ushindi


Wakati CCM ikitaja siri ya ushindi wao katika kata 77 na ubunge wa Buyungu, Chadema imekosoa mwenendo wa uchaguzi huo mdogo, ikilia na vyombo vya dola kutowatendea haki

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema jana kuwa vyombo vya dola vilitumia nguvu kubwa kuhalalisha ushindi wa CCM

CCM imeshinda katika kata zote 77 ambapo kati ya hizo, 41 walipita bila kupingwa, huku pia mgombea wao Christopher Chiza akishinda ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma

Akijibu swali baada ya kuulizwa wamekwama wapi na kukosa ushindi katika maeneo yote, Dk Mashinji alisema, “sisi hatujakwama, utaratibu umeenda vizuri, kampeni zilifanyika vizuri na watu walijitokeza kwa wingi kupiga kura lakini baada ya kuona matokeo kwamba tumeshinda, vyombo vya dola vimeamua kuvuruga.”

Dk Mashinji alisema wananchi wanapaswa kujua kwamba chaguzi zimekuwa zikiingiliwa

“Tume ya Uchaguzi siyo huru unadhani hapo haki itatekelezwa? Ndiyo maana vyombo vya dola vinapoingilia mchakato hakuna cha kufanya,” alisema

Alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa umefika wakati wa wananchi kuchukua hatua badala ya kuendelea kulalamika kila kukicha

“Wananchi lazima wahakikishe wanazuia na kudhibiti vyombo vya dola, si muda wa kulalamika tena, wasikubali kuonewa, lazima wachukue hatua.”

Vilevile Dk Mashinji alisema hatua nyingine inayopaswa kuchukuliwa ni wananchi wenyewe kumwajibisha mtu atakayekubali kutangazwa mshindi wakati hastahili

“Wananchi wasikate tamaa, adui namba moja ni aliyetangazwa mshindi ilihali hakushinda. Ni rahisi sana, hawa watu wanaishi katika jamii zetu. Kwa mfano sisi Wasukuma watu wanaofanya makosa tunawatenga na kuwapa adhabu kali za kijamii,” alisema katibu huyo

“Wasihangaike na polisi, wahangaike na wagombea, itafika mahali hata wakitaka kuwapa ushindi wa hila wataogopa kuukubali.”

Dk Mashinji alisema wananchi wenyewe wanapaswa kujua thamani ya vyama vingi kuwa kutokubali kuburuzwa

Akizungumzia uchaguzi huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Jimson Sanga alisema kwa muda mrefu vyama vya upinzani vimeshindwa kufuata taratibu za kisheria pindi vinapofanyiwa mambo yasiyopaswa na kubaki kulalamika

“Kama wana malalamiko na kuona wameonewa ni vizuri sasa wakafuata taratibu kwani chaguzi zinaongozwa na sheria, wafuate utaratibu wa kwenda katika vyombo vya maamuzi kama mahakama na kuonyesha vielelezo vyote ambavyo vitawasaidia,” alisisitiza

Hata hiyo, Sanga alisema endapo wapinzani hawana malalamiko na chaguzi zimefanyika kwa haki, ni wazi kwamba sasa Serikali imeamua kujibu ajenda zao, hivyo wanapaswa kujipongeza kwa hilo
“Wajitathmini na kuangalia nini hasa kimetokea, kama wanaamini hawakutendewa haki na wana ushahidi wa hilo waende hata mahakamani wakadai stahili yao,” alisema

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM jijini Dar es Salaam, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally alisema wamewapa matumaini wananchi kiasi cha kuaminiwa na hivyo kushinda uchaguzi huo

“Ninashawishika kusema tumeanza kufanya kazi inayowapa watu matumaini hasa wanyonge. Kila tulipopita tunazungumza lugha za matumaini na pengine tukikuta kero tunatatua,” alisema

Dk Bashiru aliongeza kuwa kila walipopita katika mikutano yao walihimiza mshikamano na kukirudisha chama hicho kwenye misingi ya Azimio la Arusha pamoja na Mapinduzi ya Zanzibar

Alitaja siri nyingine kuwa ni ya kuwatumia viongozi wastaafu akiwamo aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Yusufu Makamba

“Tumefanya mikutano ya nje na ndani. Mimi nimefanya mikutano 25 ya ndani, nimezungumza na viongozi wa dini 11 na mtu mmoja mmoja,” alisema

Akizungumzia vyama vya upinzani, alisema hawakuwa wamejipanga badala yake waliishia kupiga porojo kwenye mitandao ya jamii

“Ni wakati muhimu kujiuliza ni aina gani ya siasa tunazofanya. Tujiulize ni wapi tulipotoka na tunapokwenda. Napenda kuwashukuru Watanzania kwa imani yao na tutaitumia kuwalipa. Hatutadeka wala kubweteka,” alisema Dk Bashiru

Aliongeza kuwa, “tunawaahidi utumishi wa uadilifu, tutatumia rasilimali za nchi kwa manufaa yao.”

Katika Jimbo la Buyungu mgombea wa CCM, Chiza alipata kura 24,578 akifuatiwa na mgombea wa Chadema aliyepata kura 16,910

Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Lusubilo Mwakabibi alimtangaza Chiza baada ya kuwashinda wagombea wengine kutoka Demokrasia Makini aliyepata kura 11; UMD 12; NRA 17; UPDP 18; DP 22; AFP 51 na ACT - Wazalendo 100

Kwa mujibu wa msimamizi huyo ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kakonko, idadi ya watu waliojiandikisha ni 61,980, lakini waliopiga kura walikuwa 42,356 huku kura halali zikiwa 41,841 na zilizoharibika 515

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Chiza alisema yuko tayari kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo na kuwaahidi utumishi uliotukuka

Alisema wananchi wa Buyungu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji ufumbuzi na akishaapishwa ataanza nazo

“Kazi ya mbunge ni kujua matatizo ya wananchi na kuhakikisha anayafikisha kwa wale wanaoweza kuyatatua na kurejesha majibu anayoyapata kwa wapigakura,” alisema mbunge huyo mteule

Kwa upande wa kata, CCM imejihakikishia ushindi katika kata 41 baada ya wagombea wake kupita bila kupingwa. Hata hivyo kwa kata zilizosalia zote zilikwenda chama hicho baada ya wagombea wake kutangazwa washindi wa uchaguzi uliofanyika juzi

Imeandikwa na Tausi Mbowe, Elias Msuya, Hapioness Tesha na Muhingo Mwemezi

Chadema waelezea kilichowanyima ushindi Chadema waelezea kilichowanyima ushindi Reviewed by KUSAGANEWS on August 14, 2018 Rating: 5

No comments: