Chadema kimesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) inapaswa
kulaumiwa kwa kuvuruga uchaguzi mdogo uliofanyika Agosti 12, 2018,
kuorodhesha baadhi ya matukio iliyodai yalilenga kuwakandamiza wagombea
wa chama hicho na wanachama
Leo Alhamisi Agosti 16, 2018 chama hicho kimetoa taarifa kwa
vyombo vya habari na kubainisha kuwa baadhi ya maeneo wagombea wake
walienguliwa katika mazingira ya kutatanisha, hata walipojaribu kuhoji hakuna
hatua zozote zilizochukuliwa
Katika uchaguzi huo kwenye jimbo la Buyungu na kata 36, CCM
kiliibuka na ushindi huku vyama vya upinzani vikishindwa kuibuka na ushindi katika
kata zote na jimbo hilo.
Chama hicho kimesema
taarifa iliyotolewa na NEC kujibu tamko la Ubalozi wa Marekani
kuhusu uchaguzi huo mdogo, haiakisi ukweli wa mambo na badala
yake ilipotosha kuhusu kilichotokea kwenye mchakato wa uchaguzi huo
Taarifa hiyo iliyotolewa na ofisa habari wa chama hicho,
Tumaini Makene inasema NEC imeshindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki,
kutokana na ama kutokuwa na uwezo au kufumbia kwa makusudi hila na njama
zilizokuwa zikifanyika kuharibu na kuvuruga uchaguzi huo
“Jamii ya watanzania, jumuiya ya kimataifa na dunia nzima
iliona na kushuhudia kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari ikiwemo
vyombo vya habari na mitandao ya kijamii jinsi ambavyo NEC ilishindwa kusimamia
uchaguzi uwe huru na haki,” imesema
“Mathalani wagombea udiwani wa Chadema katika kata
tano Tunduma walinyimwa fomu zao za kugombea kwa makusudi kabisa kisha fomu
hizo wakapewa watu wengine (wanaodaiwa hawajulikani).”
Imesema, “kwa kutumia mbinu za kijinai zinazohusisha
kughushi. Kama hiyo haitoshi wagombea wetu wakaanza kusakwa na kukamatwa na
polisi na kubambikiwa tuhuma za jinai.”
Mbali na hoja hizo, Chadema imesema imeshangazwa na namna
NEC ilivyohoji Marekani ilitumia utaratibu gani kupata taarifa ilizotoa kuwa
uchaguzi uligubikwa na vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi
“Swali hilo la NEC linaibua swali jingine, je mamlaka
zilizoharibu na kuvuruga uchaguzi huo zilifanya hivyo kwa sababu zilijua hakuna
waangalizi wa kimataifa? Je zilifanya hivyo kwa sababu zilijua habari za
matukio hayo hazitaufikia ulimwengu ambao hautakaa kimya,” imesema taarifa hiyo
Hata hivyo, jana Agosti 15, 2018 NEC iliutaka ubalozi huo
kuthibitisha inachokieleza juu ya uchaguzi huo, ikisema uchaguzi mdogo huwa
hauna waangalizi wa kimataifa na kuhoji ubalozi huo umetoa wapi taarifa hizo na
hayo iliyoyaona ni kwa kutumia utaratibu upi na sheria ipi
Chadema iyashangazwa namna NEC ilivyohoji Marekani
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 16, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment