Baada ya ma-DC Jafo awageukia ma-DED

Siku moja baada ya kukemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo na kuwaweka watu ndani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amewageukia wakurugenzi watendaji wa halmashauri.

 Amewataka wakurugenzi wapya kuepuka kujiingiza katika ugomvi wa kisiasa utakaokuwa chanzo cha kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi

Jafo akizungumza na wakurugenzi watendaji wapya wa halmashauri jijini Dodoma jana, aliwataka kuepuka kujiingiza katika makundi ya kisiasa na ugomvi usioeleweka ambao utawafanya kushindwa kutekeleza majukumu yao

Wakurugenzi hao jana walikula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa watumishi wa umma

“Simamieni mipaka yenu ya kazi, kila mtu akisimamia mipaka yake kutakuwa hakuna migongano. Ninyi mnaenda huko kwa ajili ya utekelezaji wa ilani ya CCM na hakuna mjadala mwingine,” alisema

Waziri Jafo alisema, “Msiende kujiingiza katika makundi ya kisiasa na magomvi yasiyoeleweka inawezekana huko mnakokwenda kuna makundi ya kisiasa yanayogombana. Inawezekana huko mnakoenda kuna watu wanagombana simamieni ilani

“Leo hii unaenda katika halmashauri unamkuta mkurugenzi kivyake, mwenyekiti wa halmashauri kivyake, mbunge kivyake, wakuu wa wilaya kivyao.”

Alisema jambo hilo linafanya halmashauri nayo kwenda kivyake, hivyo utekelezaji wa ilani kuwa mgumu. Alisisitiza uhusiano mwema kazini na ushirikiano akisema, “Kuna baadhi ya watumishi wewe umefika pale ni mgeni, mtu mwingine anakupiga dozi ya sumu iliyokolea hata wengine huwajui kwa sura unaanza kuwachukia.”

Aliwaagiza kutenda haki kwa watu wote na kusimamia miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinajibiwa kwa wakati

Juzi, Jafo alikemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo na kuwaweka watu ndani, akisema inasababisha wananchi kuichukia Serikali

Akizungumza wakati wa kikao kazi na wakuu wa wilaya 27 walioteuliwa hivi karibuni kilicholenga kuwapa maelekezo, aliwataka kuhakikisha wanasoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ili kufanya kazi kwa weledi. “Msiende kuwa vyanzo vya migogoro kwenye wilaya zenu, tumekuwa tukishuhudia migogoro baina ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, makatibu tawala na wabunge. Hatuwezi kwenda hivi, katengenezeni Serikali,” alisema Waziri Jafo

Ujumbe wa katibu mkuu Jafo akisema hayo, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mussa Iyombe aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha wanatenga muda wa kuzungumza na watumishi badala ya kuwaachia maofisa utumishi ambao wamekuwa wajeuri

“Tunapata tabu sana, mkurugenzi haingii ofisini. Ukimtafuta humpati sasa wewe umepewa halmashauri halafu unatafutwa na waziri hupatikani, unatafutwa na katibu mkuu hupatikani, unafanya kazi gani sasa?” alihoji

“Katika muda wote niliokaa hapa, wakurugenzi hawana urafiki na watumishi. Wanaishia kwa maofisa utumishi, maofisa utumishi wajeuri kwelikweli wanawaharibia sifa lazima mkawaangalie.”

Alisema hali hiyo imewafanya watumishi kusafiri safari ndefu kwenda kumuona waziri wa Tamisemi wakati shida zao zingeweza kumalizwa na mkurugenzi

Baada ya ma-DC Jafo awageukia ma-DED Baada ya ma-DC Jafo awageukia ma-DED Reviewed by KUSAGANEWS on August 16, 2018 Rating: 5

No comments: