Wabunge waombwa kupinga marekebisho ya sheria TLS

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimesema kitawatumia wabunge wao kupinga muswada wa marekebisho ya Sheria ya TLS, yaliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Aderladus Kilangi

Katika kutekeleza azma hiyo rais wa TLS, wakili Fatma Karume kupitia barua yake aliyoiandika kwa wanachama wote akiwaelezea kuwapo kwa muswada huo ametoa wito kwa wanachama kuwatumia wabunge hao kupinga marekebisho hayo

Fatma katika barua hiyo anasema muswada huo wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa 2018 kifungu cha 108, kinalielekeza Baraza la Uongozi la TLS lililochaguliwa kuwasiliana na AG kwanza kabla ya kutengeneza kanuni mpya

Anasema AG ambaye pia ni mwanachama wa chama hicho, kwake huo ni mfano wa mwanachama mmoja kutumia mamlaka ya Bunge kujipa haki na mamlaka ndani ya jumuiya ya kidemokrasia

Katika kifungu cha 106(2)(a) cha muswada huo, wanachama wa TLS ambao si raia wa Tanzania wanazuiliwa kuchaguliwa katika Baraza la Uongozi. Vilevile katika kifungu cha 106(3) kinawazuia wanachama ambao ni watumishi wa umma, madiwani, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa kuchaguliwa katika Baraza la Uongozi

Katika kifungu cha 107 cha muswada huo, wajumbe wa Baraza la Uongozi wanazuiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa

Fatma anasema mambo hayo yanayoweka zuio kwa wanachama wa chama hicho yanayopendekezwa na AG yaliyoingizwa katika kanuni za uchaguzi za TLS, ambayo sasa yameingizwa bungeni yalikataliwa na TLS katika mkutano wake mkuu

“Mtizamo wangu wa awali kama rais wenu ni kwamba marekebisho ya Dk Kilangi ni ya kibaguzi hivyo yanakinzana na masharti ya Ibara ya 13(1) na 13(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Fatma anasema ataiomba Sekretarieti ya TLS kuitisha mkutano wa Baraza la Uongozi kujadili hatua za kuchukua kwa maslahi ya wanachama akiwamo AG.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Fatma alisema wana imani wabunge hawatakubali kupitisha sheria hiyo ambayo ni ya kibaguzi inayokiuka Katiba

Alisema kushiriki masuala ya kisiasa ni haki yao ya msingi kwa mujibu wa Katiba na kwamba, haiwezi kuchukuliwa na mtu yeyote.

Akitoa maoni yake kuhusu marekebisho hayo, wakili Juma Nassoro alisema hana shida na wanachama kutokujihusisha na masuala ya siasa, lakini tatizo haijafafanuliwa au kutolewa tafsiri ya wazi ya kujihusisha na siasa

Naye wakili Daimu Halfani alisema muda na namna ambavyo marekebisho hayo yanafanywa yanaondoa maana halisi, badala yake picha inayojengeka ni kwamba Serikali inalenga kuwabana wapinzani ambao ni wanasheria na kuwadhibiti wanasheria kwa ujumla

Halfani alisema tatizo lingine katika marekebisho hayo ni kutokuwekwa mpaka katika kujihusisha na masuala ya kisiasa, kufanya shughuli za kisiasa na kutoshirikisha wanachama katika mapendekezo hayo
Naye wakili Fulgence Massawe alisema kuna mikataba inayolinda mawakili inataka wawe huru, lakini inavyoonekana Serikali ni kama inataka kuidhibiti TLS 
Wabunge waombwa kupinga marekebisho ya sheria TLS Wabunge waombwa kupinga marekebisho ya sheria TLS Reviewed by KUSAGANEWS on July 04, 2018 Rating: 5

No comments: