Siku moja baada ya aliyekuwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara
kutangaza kurudi CCM, mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye
ametoboa siri ya sakata hilo
Kuongezea alichosema Sumaye, viongozi wengine wa Chadema
wamesema Waitara amekimbia kuhojiwa na kamati ya maadili
“Waitara alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, yote
aliyoyasema angeweza kuyahoji vikaoni, lakini hakufanya hivyo. Waitara
ameondoka kipindi ambacho kamati kuu imempa adhabu lakini si ya kumfukuza,”
alisema Sumaye jana alipozungumza na Mwananchi
Hata hivyo, Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa muongo
mmoja kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 katika utawala wa Awamu ya Tatu, alisema
hawezi kumlaumu Waitara kwa uamuzi wake huo
“Siwezi kumlaumu kwa uamuzi wa kuhama, hata mimi nilihama
CCM na kujiunga Chadema Agosti 22, 2015,” alisema Sumaye ambaye ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya chama hicho
Juzi, Waitara alitangaza kurudi CCM katika mkutano na
waandishi wa habari ulioitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey
Polepole uliofanyika ofisi ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam
Waitara aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Dar es Salaam
alitaja sababu za kuchukua hatua hiyo kuwa ni pamoja na matumizi ya ruzuku
kutowekwa bayana na uenyekiti wa Freeman Mbowe kutofika mwisho
Akifafanua hoja hizo jana alipozungumza na Mwananchi,
Waitara alisema suala la ruzuku limekuwa tatizo
“Hakuna anayeruhusiwa kuhoji, Mbowe pekee ndiye anajua
matumizi yake, anajua fedha anazipeleka wapi,” alidai
Alipoulizwa iwapo aliwahi kuhoji katika vikao vyovyote vya
chama alijibu, “Mimi si mjumbe wa Kamati Kuu, lakini Mbowe hataki kuachia
uenyekiti kwani ananufaika nao, anajua akitoka atakayekuja anaweza kufanya
ukaguzi na kumtia hatiani.”
Kuhusu hilo, Sumaye alisema, “Waitara angeweza kuuliza suala
la ruzuku katika vikao kwamba ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali) ijadiliwe, lakini hakufanya hivyo
“Hilo la Mbowe kuongoza, Waitara nalo angeweza kulileta
Kamati Kuu (ya Chadema) na kuhoji uenyekiti wa Mbowe lakini hakufanya hivyo na
sababu alizozitoa anazijua yeye kwa malengo yake ili kuhalalisha hicho
anachokitaka.”
Alipoulizwa chanzo cha Waitara kupewa adhabu ni nini, Sumaye
alisema, “Siwezi kwenda kwa undani kwani hilo lilikuwa la Kamati Kuu na
alipelekwa kamati ya maadili ambayo mimi sikuhudhuria na hata ningekwenda
nisingeweza kulizungumzia
Siri nyingine
Sababu nyingine inayodaiwa kuwa huenda ilikuwa chanzo cha
Waitara kuchukua hatua hiyo ni juu ya tetesi za kushughulikiwa jimboni kwake
“...Katika uchaguzi ngazi ya chini ya chama, waliwaondoa
watu wangu wote na kupanga safu yao
“Wamefanya hivyo ili nikose nguvu ndani ya chama ili nami
nimpigie magoti Mbowe mwaka 2020 kama nitashindwa kushinda, sasa hili
limenishinda,” alisema Waitara
Sumaye akizungumzia hilo alisema, “Kusema watu wangu, hiyo
ndiyo kasoro na kosa kubwa.Unaposema watu wangu ni kosa, chama chochote
wanachama au viongozi ni wa chama na si wa mtu.”
Sumaye alisema, “Sasa yeye (Waitara) alikuwa anasema kundi lake
limeenguliwa, mimi nilimweleza kwamba, katika chama hakuna viongozi au
wanachama wa watu binafsi na kama unaona hao waliochaguliwa si wako, cha
kufanya, wachukue uwe unafanya nao kazi
“Ukiwa unafanya nao kazi mwisho mtakuwa katika mrengo mmoja
na mimi nafikiri Waitara alianza kufanya hivyo na matokeo yalionekana sasa
sijui kilichotokea jana (juzi) cha yeye kuhama,” alisema Sumaye aliyewahi kuwa
mbunge wa Hanang’
Amekimbia kabla ya kujieleza
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa
Chadema, John Mrema akizungumzia na Mwananchi jana kuhusu Waitara kupewa adhabu
alisema, “Ni kweli alijadiliwa na kamati kuu na aliandikiwa barua
aliyokabidhiwa juzi (Julai 27) ya tuhuma zake na kutakiwa kujieleza mbele ya
kamati ya maadili taifa
“Ameamua kukimbia na sasa haelezi ukweli ila anatunga
propaganda mpya,” alisema Mrema
Alisema, “Nilimpokea Waitara kwenye chama 2008 ameamua
kuondoka, namtakia safari salama huko aendako na ndoto zake za kuwa mwenyekiti
wa chama cha siasa huenda zikatimia huko CCM, ngoja nijipe muda.”
Waitara alipotafutwa kuzungumzia adhabu aliyopewa alisema,
“Hilo la adhabu ndiyo kwanza nalisikia kwako, sijawahi kupewa barua au kuitwa
nami nilikuwa nakwenda ofisi za chama mbona sikuwahi kuelezwa na wala sijawahi
kuvuliwa uongozi wowote?”
Mrema akizungumzia hoja aliyoitoa Waitara ya ruzuku na
uenyekiti wa Mbowe alisema ni mufilisi kwa kuwa taarifa za matumizi ya fedha
zinakaguliwa na mkaguzi wa ndani na CAG ambaye ripoti zake huwekwa wazi
“Mbowe si katibu mkuu wa chama, bali ni mwenyekiti. Katibu
mkuu ndiye ofisa maduhuli wa chama, Waitara anamrukia Mbowe ili kumchafua,
tunajua wana CCM wengi hawapendi kuona Chadema imara chini ya uongozi wa
Mbowe,” alisema
Segerea kwafukuta
Wakati hayo yakitokea, Chadema Wilaya ya Ilala imetoa onyo
kwa wanachama wake 13 akiwamo Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest ambao
watakuwa chini ya uangalizi kwa miezi 18
Mbali ya wanachama hao, aliyekuwa Mwenyekiti wa Segerea,
Gango Kidera amefukuzwa uanachama, huku Katibu wa Kata ya Kinyerezi, Alex
Massaba na mwanachama mwingine, Lillian Wassira wakifikishwa mbele ya kamati ya
maadili
Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Makongoro Mahanga alisema hatua
hiyo inatokana na viongozi na wanachama kukiuka katiba na maadili ya
chama.</p></div><div><p>“Tunataka kurejesha nidhamu ya
chama. Chama kisipokuwa na nidhamu hata Ikulu tunaweza kuisikia tu. Kwa hiyo,
hawa wamechukuliwa hatua kwa mujibu wa katiba,” alisema Mahanga aliyewahi kuwa
naibu waziri wa Kazi na Ajira
Alisema watakaokuwa chini ya uangalizi hawatapaswa kurudia
makosa na hawatagombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama
Kuhusu kuondoka kwa Waitara, Makongoro alisema, “Ameondoka
kipindi ambacho anatakiwa kujibu tuhuma. Waitara alikuwa ameshavuliwa uenyekiti
wa wabunge wa Kanda ya Pwani na uenyekiti wa Greater Dar es Salaam (Dar es
Salaam Kuu
“Uamuzi huu ulichukuliwa na kikao cha kamati kuu ambacho
kimekaa kama wiki mbili zilizopita, Waitara alikuwa anajua lakini kama anasema
alikuwa hajui, hilo ni yeye. Ukweli hatua zilikuwa zimechukuliwa na barua
amepewa,” alisema
“Unajua watu wanapewa barua wanakimbiakimbia hata sisi huku
Segerea tuliowachukulia hatua wanakwepa kupokea barua lakini Waitara anafahamu
hatua zilizochukuliwa,” alisema Mahanga aliyewahi kuwa Mbunge wa Segerea kwa
tiketi ya CCM
Sumaye atoboa siri ya Waitara kutimkia CCM
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 30, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 30, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment