RC Mnyeti ageuka Mbogo Mkutanoni


MKUTANO wa hadhara  wa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti,  umegeuka kaa la moto kwa watumishi wa kujitolea wa Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Mji wa Babati  na wengine kujikuta vibarua vyao vikiota nyasi

Katika mkutano wake uliofanyika uwanja wa Kwaraa mjini hapa juzi Mnyeti alidai kukerwa na malalamiko mengi ya wananchi yaliyotawala mkutano huo kwa asilimia 98

Hali hiyo ilimfanya Mnyeti kumuagiza Mkurugenzi  Mtendaji  wa Mji wa Babati,  Fortunatus Fwema,  kuwatimua  kazi mara moja watumishi wote wa Idara ya Ardhi  wanaojitolea  ili wabaki  waajiriwa ambao serikali itakuwa rahisi kuwawajibisha

“Watumishi wote wa Ardhi, mkurugenzi waondoe, siwataki…wabaki waajiriwa na siyo wa kujitolea, maana hawa wote wanaomba rushwa na ukiona nimefanya hivyo nimefanya utafiti nikabaini wanakula rushwa

“Niliowatuma  kufanya upelelezi  nao waliombwa rushwa,  mimi wala siogopi kuwaondoa,  kabla sijaondolewa  mimi nawaondoa ambao ni ‘saizi’ yangu na kabla sijatumbuliwa ninawatumbua  wa chini yangu,’’ alifoka

Aidha, alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kumhamisha kazi mara moja mtumishi mmoja wa ardhi ambaye analalamikiwa na wananchi

Katika hatua nyingine, Mnyeti aliagia  “Mkurugenzi  rahisisha  masharti ya kupata hati maana upatikanaji wa hati umekuwa kama vile mtu kwenda Mbinguni,  huku wataalam wako wakijifanya miungu-watu  na kuwapoka haki wananchi  wanaohitaji hati zao,’’ alisema
Aidha aliwaonya wataalam wa ardhi wanaowatoza fedha wananchi na akataka kuambatana na wataalam hao kwenda kuona viwanja vinavyofanyiwa uthamini akidai kuna harufu ya rushwa

Mnyeti aliwataka wananchi waliochukuliwa ardhi yao lakini halmashauri imeshindwa kuwalipa fidia kwa muda sasa warudi kwenye ardhi zao

Akizungumzia maamuzi ya Mnyeti, mkazi mmoja wa hapa,  Peter Sulle, alimpongeza kwa hatua alizochukua za kuwaondoa wataalam waliokuwa wanawaibia  watu

Pia alisema agizo la kurudishwa maeneo yao baada ya halmashauri kushindwa kuwalipa fidia ni uamuzi wa busara

Naye Neema John, alisema, maagizo ya Mnyeti yanapaswa kutekelezwa kwani baadhai ya watumishi hawawezi kufanya kazi bila kusukumwa
RC Mnyeti ageuka Mbogo Mkutanoni RC Mnyeti ageuka Mbogo Mkutanoni Reviewed by KUSAGANEWS on July 28, 2018 Rating: 5

No comments: