Wanafunzi wanne wafa Maji Dar


Wanafunzi wanne wa kidato cha nne katika Sekondari ya Kimbiji jijini Dar es Salaam wamefariki dunia baada ya kuzama katika ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Kimbiji

Waliofariki wametajwa kuwa ni Queen Madala (16), Selestina Malipesa (16), Cecilia Ernest (17) na Agneta Philipo (17).

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi jioni wakati wanafunzi hao wakiogelea ufukweni baada ya kupelekwa na walimu wao

“Walimu waliamua kuwapeleka wanafunzi hao wa kidato cha nne ili kuwapongeza wenzao waliofanya vizuri katika mitihani ya mock (majaribio),” alisema Lukula

“Walikuwa na vyakula na michezo mbalimbali, lakini baadaye waliingia kuogelea ambapo hao wanne walizidiwa nguvu na maji na mmoja alifariki hapohapo na wengine hadi kufikishwa Kituo cha Afya Kimbiji daktari alithibitisha kufariki kwao.”

Alisema walioshuhudia walisema wanafunzi hao walipoanza kuzidiwa nguvu na maji walikuwa wakitapatapa ndipo wenzao walipiga yowe ya kuomba msaada

“Wenzao wanaojua kuogelea, wakisaidiana na walimu na watu waliokuwa katika maeneo hayo walifanya jitihada za kuwatoa majini kabla ya gari ya wagonjwa kufika na kuwakimbiza kituo cha afya,” alisema Lukula

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya mahojiano na walimu wao ili kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kufahamu ni kwa sababu gani waliwapeleka wanafunzi hao ufukweni bila ya kuwa na tahadhari

“Pasipo kutambua kuwa unapopeleka watoto wengi ufukweni kuna miongoni mwao wanajua kuogelea na wengine hawajui, ila wao walisahau kuliangalia hilo na kuruhusu wanafunzi wote kuingia kwenye maji.”
Wanafunzi wanne wafa Maji Dar Wanafunzi wanne wafa Maji Dar Reviewed by KUSAGANEWS on July 31, 2018 Rating: 5

No comments: