Meli 21 zakamatwa kwa uvuvi haramu, zatozwa faini


Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekamata meli 21 na kuzipiga faini ya Sh1 bilioni kila moja baada ya kubainika kufanya uvuvi haramu katika ukanda wa bahari kuu

Hayo yameelezwa leo Jumapili Julai Mosi, 2018 na waziri wa wizara hiyo, Luhaga Mpina wakati akizindua menejimenti itakayosimamia Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico

“Kati ya meli hizo 21 tulizozikamata, 19 zilitoroka ukaguzi lakini tulifanikiwa kuzikamata na kuzipiga faini ya Sh1 bilioni kwa kila meli, hii ni rekodi kwa mara ya kwanza tangu nchi yetu ipate uhuru kukamata meli nyingi,” amesema Mpina.

Amefafanua kuwa watoza faini hizo ni Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu na si waziri

“Pia kuna meli ya Buhanaga 1 kutoka China, nayo ilikamatwa mwishoni mwa Januari mwaka huu, ikiendesha uvuvi haramu ukanda wa bahari kuu na tuliipiga faini ya Sh770 milioni na tuliwapa siku saba kulipa faini hiyo lakini hawakulipa,” amesema

“Tukawaongezea muda pia hawakulipa, kwa sasa meli hiyo inashikiliwa na Serikali, ikiwa na tani 32 za samaki na tayari mmiliki, wakala na nahodha wa meli hiyo wamekamatwa na kufunguliwa kesi mkoani Mtwara.”

Amesema kutokana na udhibiti wa utoroshaji wa samaki na uvuvi haramu walioufanya, mapato yameongezeka maradufu na kufikia Sh10 bilioni kwa kipindi cha miezi sita, huku mwaka wa fedha 2016/2017, wizara hiyo ikikusanya mapato ya Sh18bilioni
Meli 21 zakamatwa kwa uvuvi haramu, zatozwa faini Meli 21 zakamatwa kwa uvuvi haramu, zatozwa faini Reviewed by KUSAGANEWS on July 01, 2018 Rating: 5

No comments: