Maisha ya Arusha na kilio cha kudorora Tanzanite


Kushuka ghafla kwa mapato yatokanayo na madini ya Tanzanite kutoka Sh444 milioni hadi Sh40 milioni kwa mwezi kumeanza kuwaathiri wakati wa Arusha na Mirerani kutokana na kupungua kwa mzunguko wa fedha, Mwananchi linaripoti

Wiki iliyopita mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na wajumbe wake walitembelea mgodi wa Mirerani na kuwaambia waandishi wa habari kuwa wamebaini utoroshaji wa Tanzanite uliosababisha kushuka mrabaha kutoka Sh444 milioni hadi Sh40 milioni kwa mwezi

Alisema wamebaini kuwapo udanganyifu unaofanywa na madalali wanaonunua madini migodini. “Madalali hawa wakitoka kununua madini wamekuwa wakipita getini, baadhi wanahofiwa kuficha madini hasa kutokana na kukosekana vifaa vya kisasa vya upekuzi,” alisema Profesa Kikula

Licha ya ujenzi wa ukuta kuzunguka migodi ya Tanzanite, Profesa Kikula alisema pamoja na sababu nyingine wanaamini kuna utoroshwaji wa madini hayo

Maisha ya wananchi Uchunguzi wa Mwananchi katika mji wa Arusha na Mirerani umebaini kuwa biashara kadhaa zimeanza kukosa wateja huku hali hiyo ikijidhihirisha wazi katika maisha ya wakazi wa maeneo ambayo wachimbaji wamekuwa wakikutana

Hali katika baadhi ya klabu za starehe, hoteli na maeneo ya kuuza madini imeanza kubadilika kutokana na kupungua kwa wateja

Uchunguzi huo umebani kupungua kwa kiasi kikubwa cha wateja katika klabu maarufu ambazo siku za nyuma zilikuwa ‘zikijaza’ wateja hata siku za mwishoni mwa wiki
Jeremiah Mollel, mfanyabiashara mjini Arusha anasema kudhibitiwa kwa biashara ya madini kumechangia kupungua wateja

Katika eneo la jengo la OTTU na maeneo ya St Thomas, ambapo kawaida huwa na idadi kubwa ya wauzaji wa madini, pia watu wamepungua sana kutokana na kukosekana kwa madini

Dalali wa madini, Raphael Wandiba anasema baada ya biashara ya Tanzanite kuwa ngumu, madalali wengi wamehamia migodi ya Ruby wilayani Longido

“Hapa biashara ni ngumu sana, hakuna madini ya Tanzanite ambayo yanafika mjini,”alisema

Hali ya maisha katika maeneo kadhaa ya mji wa Mererani imeanza kuwa ngumu kwa kile wakazi wanachoeleza kuwa ni kutokana na kudhibitiwa madalali wa madini na wafanyabiashara wengine kuingia migodini

Peter Kaaya anasema tofauti na siku za nyuma, sasa mzunguko wa fedha katika mji huo umepungua sana. “Mtu kukupa hata Sh5,000 imekuwa ni ngumu. Zamani ukiomba mtu atakupa hata Sh50,000 lakini sasa kila mtu ana hali ngumu, nadhani udhibiti wa biashara ya madini umechangia,”alisema

Mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji wa Madini Tanzania (Tamida), Sammy Mollel anaamini kuwa mapato ya Serikali yameshuka na hali ya maisha imekuwa ngumu kutokana na uzalishaji wa madini kupungua

Anasema Tamida ilipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya Tume ya Madini kuwa kushuka kwa mapato kumetokana na utoroshwaji wa madini. “Sisi tunachojua ni kwamba uchimbaji umedorora na hata kama bado kuna watoroshaji usingesababisha pengo kubwa la mrahaba

“Hata kama kungekuwepo utoroshwaji wa madini hayo, haiwezekani kwa mwezi kusababisha hasara ya milioni 400, sisi tunaamini uzalishaji madini umeshuka na migodi mingi imesimama,” anasema

Anasema hali hiyo haiathiri Serikali tu, bali hata wachimbaji na wananchi kwani kuna zaidi ya watu milioni moja katika jiji la Arusha na Mirerani wanaotegemea biasara ya Tanzanite

“Serikali inachopaswa kufanya sasa ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata wataalamu na teknolojia za kisasa za kuchimba madini lakini pia mabenki yaanze kutoa mikopo kwa wachimbaji wa madini,”anasema

Anasema Serikali inapaswa kufanya tafiti za kina katika migodi ili kujua maeneo yenye madini na kujua yapo umbali gani ili kurahisisha uchimbaji jambo ambalo litafanya Serikali kupata mapato

Anasema sababu ya pili ya kushuka mrahaba wa Serikali ni kuwa zaidi ya migodi 10 iliyokuwa inachimbwa katika eneo la Kitalu B na D ambalo lipo mpakani na kitalu C kinachomilikiwa na Tanzanite One imesimamisha uzalishaji

“Uchimbaji umesimama kutokana na makubaliano ambayo yalifikiwa na pande zote kufanya uchimbaji kwa kushirikiana hasa katika maeneo ya mgogoro na sasa kutokana na Tanzanite One kusimamisha uchimbaji imekuwa ngumu hata migodi mingine kufanya kazi,”anasema

Mmoja wa wakurugenzi wa Tanzanite One, Faisal Shabhai anakiri kuwa shughuli za uchimbaji Tanzanite One zimesimama na kwamba zitaanza siku chache zijazo.</p></div><div><p>Katibu wa wachimbaji Mirerani, Abubakar Madiwa anasema hali ya maisha kwa wakazi wa Mirerani wanaotegemea madini ni ngumu, kwani biashara nyingi zimesimama na hakuna mzunguko wa fedha

“Hapa kuna akinamama ambao huingia migodini kuuza vyakula, kuna wafanyabiashara wa maji, kuna madalali wa vichenga vya madini, sasa ghafla kuwazuia hawa wote kuingia ni tatizo,” anasema

Anasema wao hawawaungi mkono wanaotaka kutorosha madini bali wanachotaka ni kuona Serikali inakusanya mapato yake na wananchi wananufaika moja kwa moja na madini yao

Wachimbaji wengine wanaamini kuwa kushuka kwa mrabaha pia kumechangiwa na baadhi ya wamiliki wa migodi na madalali kubaini mbinu mpya ya kukwepa kuilipa Serikali na kutoroshwa madini

Wamiliki migodi wazungumzia

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Sadick Mnenei anasema kwa ujumla uchimbaji na biashara ya Tanzanite vimedorora

Anasema taarifa ya hivi karibuni ya Tume ya Madini imefanya uchimbaji wa madini kuwa mgumu zaidi kutokana na kuongezeka kwa udhibiti wa vyombo vya usalama katika kuingia mgodini.</

“Sisi tunaamini kushuka kwa mapato ya Serikali hapa Mererani hakusababishwi kwa kiasi kikubwa na utoroshwaji madini bali kushuka kwa uzalishaji wa madini

“Sisi wamiliki wa migodi tunajua tunapoanza kupata madini biashara ya kuuza madini na maisha ya Mirerani hadi Arusha hubadilika na kuwa bora na mrabaha wa Serikali utaongezeka,” anasema

Anasisitiza kuwa madini ya Tanzanite hayawezi kutolewa kwa kificho. “Kama mgodi unatoa madini kila mtu atajua kwani kuna wachimbaji wadogo zaidi ya 50 kila mgodi… kuna wasimamizi na maofisa madini,”anasema

Anasema Marema inaunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha madini ya Tanzanite yananufaisha Watanzania wote na hivyo kuzuiwa njia yoyote ya kutoroshwa madini nje ya nchi
Maisha ya Arusha na kilio cha kudorora Tanzanite Maisha ya Arusha na kilio cha kudorora Tanzanite Reviewed by KUSAGANEWS on July 30, 2018 Rating: 5

No comments: