Madiwani walioponzwa na naibu spika kujiuzulu kujiunga na CCM


MADIWANI wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ambao walitangazwa kuvuliwa uanachama, wamewasilisha rasmi barua za kujiuzulu nafasi zao kwa Mkurugenzi wa Jiji hilo

Madiwani hao ni wale walidaiwa kukaidi maagizo ya viongozi wa chama hicho kuhusu mwaliko wa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, wa kwenda bungeni jijini Dodoma

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Dk. Amani Kilemile, aliwataja madiwani hao na kata zao kuwa ni Geofrey Kajigili (Sisimba), Newton Mwatujobe (Manga), Mchungaji David Ngogo (Nsalaga) na Humphrey Ngalawa (Iwambi

Dk. Kilemile alisema madiwani hao walianza kuwasilisha barua zao kuanzia Julai 18, mwaka huu, na kwamba diwani wa mwisho aliwasilisha Julai 25

“Kutokana na madiwani hawa kuwasilisha barua zao, natangaza rasmi kuwa kuanzia sasa si wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri yetu ya Jiji la Mbeya,” alisema Dk. Kilemile

Alisema baada ya kupokea barua hizo, amechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumwarifu Mstahiki Meya wa Jiji hilo, David Mwashilindi, kuhusu kujiuzulu kwa madiwani hao

Alisema kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, mstahiki meya anatakiwa kuwasilisha taarifa ya kujiuzulu kwa madiwani hao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa hatua zaidi na barua tayari imeandaliwa, kilichobaki ni kutiwa saini na kutumwa

Aidha, alisema kwenye barua zao, madiwani hao wameeleza sababu zinazofanana za kujiuzulu kuwa ni kutoelewana na viongozi wa chama chao na kwamba wananyanyaswa wakidaiwa kuwa ni wasaliti

Alisema madiwani hao wameeleza kwenye barua zao kuwa wameingia kwenye mgogoro na viongozi wao kutokana na kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika Jiji hilo

Julai 21, mwaka huu, uongozi wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, chini ya Mwenyekiti wake, Obadiah Mwaipalu, ulitangaza kupeleka mapendekezo katika ofisi ya chama hicho Kanda ya Nyasa kuwafuta uanachama madiwani watatu

Madiwani waliopendekezwa na chama hicho kufukuzwa ni Kajigili, Mwatujobe na  Ngallawa, ambao walidaiwa kukiuka katazo halali la chama hicho la kutohudhuria mwaliko wa Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, bungeni jijini Dodoma

Aidha, siku hiyo hiyo, Ngogo alitangaza kujivua udiwani na uanachama wa Chadema kwa kile alichodai kuandamwa na viongozi wa chama hicho baada ya kuungana na Naibu Spika kwenye shughuli za maendeleo

Hata hivyo kabla uongozi wa chama hicho haujatoa uamuzi wake, madiwani hao wameamua kuandika barua za kujiuzulu.
Madiwani walioponzwa na naibu spika kujiuzulu kujiunga na CCM Madiwani walioponzwa na naibu spika kujiuzulu kujiunga na CCM Reviewed by KUSAGANEWS on July 28, 2018 Rating: 5

No comments: