Chadema walia michango kwa Shule za Msingi ,Sekondari


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesikitishwa kuibuka  michango mbalimbali kwa shule za msingi na sekondari kwa kuwa serikali ilitangaza kuifuta.

Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema hivi sasa baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani humo wanachangishwa kiasi cha Sh. 10,000

Lema aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo katika Kata ya Mawenzi iliyopo Manispaa ya Moshi, wakati akimnadi mgombea udiwani wa chama hicho, Afrikana Mlay

Alisema anashangazwa na kitendo cha serikali kutangaza kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na tayari kumeanza kujitokeza changamoto hiyo

Alisema changamoto anayoiona ni CCM kunakili sera za Chadema, licha ya kujipambanua wanaweza kuzitekeleza lakini inaonekana kama mpango huo unataka kuwashinda.

Aidha, Lema alisema Chadema kinatoa angalizo kwa wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) juu ya zoezi la kutengenezewa vitambulisho kwa Sh. 10,000 zoezi hilo limeghubikwa na utata mkubwa na linalenga kuwatambua na kuwalipisha kodi kubwa

Alisema Chadema hawapingi zoezi la kuwatambua machinga na kuwapatia vitambulisho kwani inatambua ili wananchi waweze kupata huduma za afya ,ujenzi wa barabara na upatikanaji wa huduma za  maji ni lazima wananchi walipe kodi

Alisema kabla ya Machinga kutakiwa kulipia vitambulisho kwa Sh. 10,000 serikali ilipaswa kuwaelimisha na kuwapatia mtaji pamoja na maeneo maalumu kwa ajili ya kufanyia biashara zao kwa uhakika na usalama

“Hivi vitambulisho mnavyoaandaliwa mjiandae kutambulika mjulikane ni akina nani na mpo wangapi ili muweze kulipishwa kodi hii inapaswa kutazamwa kwa jicho la ziada ili kuweza kuwasaidia machainga kuondokana na kunyanyasika katika nchi yao”alisema Lema

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Killimanjaro, Grace Kiwelu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) alisema Chadema kimejipanga kunyakua ushindi wa kishindo kata za Makanya Same na kata ya Mawenzi mjini Moshi.

 Alisema wananchi hawana budi kuondoa hofu ya kushindwa katika uchaguzi mdogo wa marudio ya udiwani na ubunge kwa kuwa chama hicho kimejipanga kulinda kura zao kwa gharama yoyote kwani wanachama  na baadhi ya wananchi wamekuwa na hofu ya kuporwa ushindi wao katika marudio ya uchaguzi ndogo zinazoendelea hapa nchini.

Kiwelu alisema baraza la wanawake chadema na vijana mkoa Kilimanjaro watahakikisha wanalinda kura zao zote na hakuna mtu atakayeweza kupora ushindi wa umma na kubadilisha matokeo huku akitoa rai kwa tume ya uchaguzi na serikali kuhakikisha zoezi la marudio ya uchaguzi mdogo linafanyika na  linamalizika kwa uhuru na  amani

Kiwelu alisema tume ya uchaguzi haina budi kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa kufuta sheria kanuni na maadili yaliyowekwa na serikali na vyama vya siasa ili zoezi hilo liweze kumalizika kwa  amani na kuwachukulia sheria kali wale wote watakaobainika kuvunja sheria za uchaguzi
Chadema walia michango kwa Shule za Msingi ,Sekondari Chadema walia michango kwa Shule za Msingi ,Sekondari Reviewed by KUSAGANEWS on July 28, 2018 Rating: 5

No comments: