Kufuatia kuvuliwa cheo kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mwigulu Nchemba kutokana na ongezeko kubwa la ajali nchini na kuteuliwa
kwa Kangi Lugola ambaye sasa anashika nafasi hiyo, Waziri huyo mpya tayari
ameanza kazi kwa kasi hasa katika kutafuta suluhu za ajali ambazo zimekuwa
zikitokea mara kwa mara.
Ambapo amesema Serikali inajipanga kuja na mbinu mpya ya
kudhibiti na kupunguza ajali zinazosababishwa na pikipiki.
Lugola amesema Serikali itaanzisha utaratibu wa kufunga
tela katika pikipiki kwamba abiria wataweza kupanda kati ya mmoja hadi wanne na
kuketi katika tela hilo.
Kwa kufanya hivyo amesema ajali za pikipiki zitapungua
kwa kiasi kikubwa sana kwani pikipiki zikishafungwa tela zitashindwa kutembea
kwa mwendokasi mkubwa kutokana na uzito lakini pia zitashindwa kupenya penya barabarani
na kufanya vurugu.
”Tutawafungia matela ya kubeba abiria na nyie mkae kwenye
foleni kama bajaji na magari mengine. Matela haya yataleta utulivu barabarani
lakini pia yatawaongezea tija kwani badala ya kubeba abiria mmoja sasa mtapakia
zaidi” amesema Lugola
Ameongezea kuwa ufungwaji huo wa matela utahusisha zaidi
pikipiki za biashara na hautazihusu pikipiki binafsi.
”Bodaboda dawa yenu inachemka Serikali inakuja na mpango
madhubuti wa kupunguza kama si kumaliza kabisa ajali za barabarani zinazosababishwa
na madereva pikipiki,” amesema Lugola.
Lugola: Bodaboda dawa yenu inachemka, aja na mwarobaini kupunguza ajali
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 09, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 09, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment