Abiria 400 kukwea Dreamliner safari ya kwanza


ZAIDI ya abiria 400 wanatarajiwa kusafiri katika safari ya kwanza ya ndege mpya aina ya Boeing 787-800 Dreamliner kutoka Dar es Salaam- Mwanza- Kilimanjaro na kurudi Dar es Salaam

Idadi hiyo ya abiria 402 katika safari hizo mbili za uzinduzi rasmi kesho, za kwenda na kurudi, ambao walikuwa wamekata tiketi hadi juzi, ni sawa na asilimia 70.8.

Kwa safari moja, ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 284 ambao ni 262 daraja la kawaida na 22 kwa daraja la biashara. Kwa safari mbili ina uwezo wa kubeba abiria 568 kwa madara hayo mawili

Akizungumzia maandalizi ya mapokezi ya ndege hiyo mkoani Mwanza juzi, Mkuu wa Mkoa huo, John Mongella, alisema tiketi 244 zimenunuliwa kwa safari ya saa moja asubuhi na 158 kwa safari ya usiku

“Ninawaomba wananchi wa Mwanza na mkoa jirani  fursa kwa kuwahi kununua tiketi chache zilizobaki," alisema Mongella

Sambamba na wito huo, Mongella aliwataka wananchi wa mkoa huo na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, kutumia fursa ya ujio wa ndege ya Boeing 787-800 kwa maendeleo ya uchumi

Katika ujio huo kwa ndege hiyo kuanza safari za Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro, alisema usafiri wa ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) uwe kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alisema serikali imenunua ndege hiyo mpya na ya kisasa kwa lengo la kuchangia kuinua uchumi wa nchi na kwamba kwenye safari ya kwanza mkoani hapa, itapokewa rasmi uwanja wa ndege wa Mwanza, saa moja asubuhi

Mkuu wa mkoa aliwaomba wananchi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kufika uwanjani hapo kushuhudia mapokezi ya ndege hiyo

Kwa upande wake, Msimamizi wa ATCL Kituo cha Mwanza, Theonestina Ndyetabula, shirika limejipanga vizuri na linazidi kuimarika, hivyo kuwaomba wadau wa usafiri wa anga washirikiane kwa kutumia usafiri wa shirika hilo kupitia ndege zake za "Boeing 787-800 Dreamliner na "Bombadier Dash 8-Q400

"Matumaini yetu ni kufanya vizuri, kwa kipindi hiki chote cha ndege hizi hakika tutafanya vizuri. Pia hizo ndege mbili zinafanya safari katika uwanja wa ndege wa Mwanza mara nne kwa siku," alisema Ndyetabula

Kuhusu ratiba ya usafiri huo, alisema Mwanza - Dar kupitia Kilimanjaro ni saa 3:20  hadi 5:40 asubuhi kwa Dreamliner; Mwanza - Bukoba saa 5:15 hadi 5:45 asubuhi kwa  Bombadier

Alisema kwa safari za mchana, Mwanza - Dar ni saa 7:15 hadi 9:00 alasiri mchana kwa Bombadier na usafiri wa usiku Mwanza - Dar ni saa 2:20 hadi 3:40 usiku hiyo kwa  Dreamliner
Abiria 400 kukwea Dreamliner safari ya kwanza Abiria 400 kukwea Dreamliner safari ya kwanza Reviewed by KUSAGANEWS on July 28, 2018 Rating: 5

No comments: