Mbunge wa kuteuliwa AbdallaH Bulembo
amemtaka Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, kuunda Tume maalumu ya Bunge
ambayo itachunguza madhara waliyopata wananchi kutokana operesheni
mbalimbali za kuzuia uvuvi haramu nchini.
Bulembo amesema hayo leo Mei 18,
2018 Bungeni mjini Dodoma alipokuwa anachangia hoja ya kupitisha makadirio ya
mapato na matumizi ya wizara ya mifugo na uvuvi katika mwaka wa fedha 2018/2019
na kuongeza kuwa wananchi wamekuwa watumwa katika nchi yao kutokana na
kunyanyasika na operesheni hizo.
“Baada ya miezi tisa mnaenda kuomba
kura kwenye serikali za mitaa, mnaenda kusema nini kwa hali hii? mnaendaje kuongea
na watu hawa? mtanzania anakuaje mtumwa kwenye nchi yake? wafanyakazi wanalia,
wafanyabiashara wanalia, watu wote wanalia inawezekanaje, Mpina huwatendei haki
watanzania na hii kuna siku Mungu atahukumu, watu wamekuwa watumwa kwenye nchi
yao kwasababu ya kuvua” amesema Bulembo.
Mbunge huyo ameongeza kuwa Waziri wa
mifugo na uvuv Luhaga Mpina amekua kiongozi asiyependa kusikiliza shida
wanazopata wananchi kutokana na uendeshwaji mbovu wa operesheni hizo, Bulembo
amesema “wafugaji wanadhambi gani, kufuga ni dhambi? waziri anafuatwa mpaka
kwenye viwanja vya Bunge hataki kuwasilikiza watu, wewe ni waziri wa nani? kama
hauwahudumii watu uwaziri wako ni wa nini?”
Bulembo amedai kwamba hataunga mkono
hoja ya Wizara Mifugo ya Uvuvi mpaka pale itakapoundwa Tume na waziri husika
kusimamisha operesheni kwani katika operesheni hizo wapo baadhi ya watu ambao
walipigwa risasi na wengine kujinyonga.
''Watanzania ni watumwa katika nchi yao'' -Bulembo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 18, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment