Mtuhumiwa wa mauaji ambaye ni shahidi wa nane wa utetezi,
Muslim Mmbaga (35), jana aliwaacha hoi wasikilizaji katika Mahakama Kuu Kanda
ya Moshi, alipodai mtu anayedaiwa kumuua, yuko mitaani anatembea
Mmbaga ambaye aliitwa kumtetea mshtakiwa wa kwanza, Sharifu
Mohamed, alidai marehemu Sebari Kitivo Mbura ni shahidi wa mashtaka katika kesi
ya bilionea Erasto Msuya
Shahidi huyo (Mmbaga) anayeshikiliwa katika Gereza la
Karanga kwa kesi hiyo ya mauaji PI 206/2015, alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa
na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula baada ya kutoa ushahidi wake
Wakili Chavula alimtaka shahidi huyo aieleze Mahakama, huyo
marehemu anayetuhumiwa kumuua anaitwa nani, ndipo alipodai hajafa na ni
miongoni mwa mashahidi wa kesi ya Msuya
“Hakuna mtu aliyeuawa. Yuko hai na ni shahidi katika kesi
hii. Ndiyo, anaitwa Sebari Kitivo Mbura yuko hai na yuko nje huru,” alidai
shahidi huyo na kufanya wasilikizaji kuguna na kuangua kicheko
Alidai kuwa awali, kesi hiyo ilikuwa ni ya unyang’anyi wa
kutumia silaha uliotokea wilayani Same, lakini aliachiwa huru na Mahakama Mei
5, 2015 na akakamatwa tena na kushtakiwa kwa mauaji
Alipoulizwa katika kesi hiyo alikuwa yeye na washtakiwa
wangapi walioshtakiwa pamoja, Mmbaga alidai hakumbuki lakini baada ya kubanwa
sana na wakili Chavula, akasema walikuwa washtakiwa watano
Chavula alimuuliza kama anakumbuka namba ya kesi nyingine ya
unyang’anyi wa kutumia silaha huko Siha, alidai hakumbuki hadi alipokumbushwa
na wakili huyo kuwa ni CC 327/2014
Alipoulizwa inakuwaje mambo yanayomhusu ya 2014 na 2015
hayakumbuki, lakini anakumbuka ya mwaka 2013 yanayomhusu Sharifu, shahidi huyo
alidai ni kwa sababu anapenda vitu ‘vizuri vizuri.’
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka na kutakiwa
kueleza kama anavyomfahamu mke wa Sharifu kwa kuwa ni marafiki wakubwa, shahidi
huyo alidai hamfahamu mke wa mshtakiwa.
“Mshtakiwa wa kwanza
ni rafiki yangu sana. Namfahamu mtoto wake anaitwa Mohamed. Simjui mke wake kwa
sababu siyo utaratibu mzuri kwa sisi Waislamu kumjua mke wa mwenzako,”alidai
Awali, akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili Hudson
Ndusyepo, alidai anamfahamu mshtakiwa wa kwanza tangu mwaka 2009 na siku ya
tukio la mauaji ya Msuya alikuwa naye Singida
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje
ya Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7,2013 katika eneo la Mijohoroni
wilayani Hai
Mmbaga alidai mwanzoni mwa Julai 2013, alikwenda katika
machimbo ya dhahabu ya Londoni yaliyoko Ikungi Singida, baada ya kuona dhahabu
inatoka, aliamua kumuita Sharifu kama rafiki yake
“Tarehe 15.7.2013 Sharifu alinipigia simu kwenye saa 3
asubuhi akaniambia yuko njiani kuja Londoni na ilipofika saa 11 jioni alifika
na nikampokea na kumpeleka kwa mwenyeji wangu,”alidai
Mmbaga alidai kuwa siku iliyofuata walikwenda kuangalia
maeneo ya migodi yenye dalili za kutoa madini mapema na kugundua dhahabu
inapatikana ya kutosha katika machimbo hayo ya madini
“Tuliendelea na shughuli hiyo mpaka tarehe 10.8.2013 majira
ya jioni nilipoagana na Sharifu kwa vile alikuwa anarudi Arusha. Baada ya wiki
moja nikawa nampigia simu akawa hapatikani,” alidai Mmbaga
“Baada ya kupita wiki tatu kuna jamaa yangu wa Mirerani
anaitwa Munisi akanipigia simu akaniambia jamaa yako (Sharifu) kakamatwa lakini
hakuniambia amekamatwa kwa tuhuma gani
“Nilitoka Londoni Oktoba na kurudi Arusha na nilipofika
nikamtuma shemeji yangu anaitwa Magreth Mushi aende kumuona (Sharifu) gerezani.
Aliporudi aliniambia Sharifu kasema niende mwenyewe
“Nilikuja moja kwa moja mahakamani (akionyesha jengo
lililoko nyuma yake), tukaonana akanieleza mkasa uliomkuta lakini nikamwambia
asiwe na hofu kwa vile siku ya mauaji tulikuwa wote Londoni.”
Hata hivyo, alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka
walikutana na Sharifu Mahakama gani, alisema ya Wilaya ya Moshi Mjini, ingawa
aliyoionyesha kwa ishara ilikuwa Mahakama ya Mwanzo
Shahidi wa saba wa utetezi
Awali, shahidi wa saba wa utetezi, Isack David ambaye ni
mdogo wa mshtakiwa wa kwanza (Sharifu) aliieleza Mahakama namna mshtakiwa huyo,
alivyokamata na polisi nyumbani kwake, Agosti 13,2013
Shahidi huyo alidai kuwa baadhi ya vitu vya kaka yake
vilichukuliwa na polisi zikiwamo bunduki zake mbili na vitabu vyake vya
umiliki, pingu iliyokuwa nyumbani kwake pamoja na hati ya kusafiria.
Akiongozwa na wakili
Ndusyepo kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alidai siku hiyo alfajiri, alisikia
mlango wa nje ukigongwa na alipotoka kwenda kufungua, alikutana na kaka yake
sebuleni
Shahidi huyo alidai mshtakiwa alimwambia aache akafungue
yeye (Sharifu) kwa vile alikuwa amewaona kupitia kamera za usalama (CCTV), kuwa
waliokuwa wanagonga walikuwa ni polisi.
Alidai, kabla ya siku hiyo, kaka yake alikuwa amesafiri
kwenda Singida na siku hiyo hakuwa amefahamu kama alikuwa amesharejea hadi
walipokutana sebuleni akitaka kwenda kufungua mlango
Aliiambia Mahakama kuwa baada ya kaka yake kutoka nje,
alibaki ndani ghorofani na akawa anachungulia dirishani, akaona magari mawili
na yakaondoka na kaka yake
Shahidi huyo alidai baada ya hapo, aliwasiliana na wazazi
kuwaeleza hali halisi na walifika na kwenda Kituo cha Polisi Arusha na
walipofika walijibiwa kuwa hakuna taarifa zozote za mtu anaitwa Sharifu
Alidai kuwa baada ya hapo, alitoka na kuendelea na majukumu
yake na siku iliyofuata saa tano asubuhi, alipokea simu kutoka kwa mtu
aliyejitambulisha ni mkuu wa upelelezi Arusha
David alidai kuwa mkuu huyo wa upelelezi ambaye hakumtaja
kwa jina, alimtaka arudi nyumbani kwa kaka yake alipokuwa anaishi kwa kuwa
wanataka kufanya upekuzi
“Nilirudi nyumbani na nilipofika niliwakuta polisi ambao
waliingia ndani na kuomba kuingia chumba cha Sharifu. Waliingia ndani ya chumba
na kufanya upekuzi wa nyaraka zake mbalimbali
“Baada ya upekuzi walichukua vitu ikiwamo bunduki yake kubwa
na ndogo na vitabu vyake, Passport, DVR ya CCTV na pingu. DVR ilisharudishwa
lakini sijui vitu vingine viko wapi,” alida David katika ushahidi huo
Shahidi huyo ambaye alidai kuwa alikuwa akiishi na Sharifu
kuanzia mwaka 2010, alikana kumfahamu Mussa na Adamu Leani
Alipoulizwa kuhusiana na pikipiki mbili mpya zinazodaiwa
kupelekwa nyumbani kwa Sharifu na kutumika katika mauaji, shahidi huyo
alikanusha na kudai hazijawahi kupelekwa
Shahidi atoa mpya mahakamani, aeleza anayedaiwa kuuawa yuko hai mtaani
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 19, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 19, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment