Watano waliotoka jela kwa msamaha wauawa na wananchi

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema watu watano waliotoka gerezani kwa msamaha wa Rais John Magufuli wameuawa na wananchi baada ya kurejea katika matendo maovu

Sirro aliyewataka wanaoachiwa huru kwa msamaha wa rais 
kutorejea katika matendo hayo, ametoa kauli hiyo   leo Alhamisi Mei 24, 2018 mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati, Kiluvya-Gogoni na Mbweni vilivyozinduliwa leo

“Nia ya Rais Magufuli kuwapa msamaha ilikuwa njema lakini kuna baadhi ya watu wameitumia vibaya fursa hiyo na hadi sasa watu watano wamekwishauawa na wananchi,” amesema

“Ukitoka gerezani kwa msamaha, maana yake umerekebisha mwenendo wako na wananchi wanatarajia uwe hivyo, lakini kama ukifanya vinginevyo Serikali isilaumiwe.”

Akizungumzia utendaji wa jeshi hilo, Sirro amesema tangu ashike madaraka hayo polisi wamewapeleka askari 1,267 kwenye mafunzo ya medani za kivita na wako imara

Pia tumepeleka askari wa upelelezi zaidi ya 1,000 kwenye mafunzo ya ujuzi na ustadi wa kupeleleza kesi mbalimbali. Baada ya kuwapa mafunzo haya, tunataka kesi za kawaida upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi sita” amesema na kubainisha kuwa kesi kubwa upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi 12

Pia, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari, kutoa kibali cha ajira kwa askari wapya 1,500 na kuwaruhusu wawapandishe vyeo askari wenye kustahili kuanzia cheo cha koplo hadi naibu kamishna wa polisi (DCP).
Watano waliotoka jela kwa msamaha wauawa na wananchi Watano waliotoka jela kwa msamaha wauawa na wananchi Reviewed by KUSAGANEWS on May 24, 2018 Rating: 5

No comments: