Watu watatu
wanaotuhumiwa kuwa majambazi wamepigwa mawe hadi kufa na wananchi wa Kijiji
cha Bubare Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Watuhumiwa hao waliuawa baada ya kuwekewa mtego kutokana na kuwapo taarifa za
wao kutaka kuvamia nyumba ya mmoja wa wakazi wa kijiji hicho kwa nia ya
kupora fedha za mauzo ya mifugo.
Baadhi ya viongozi wa Serikali ya kijiji waliojaribu kuwazuia wananchi
kuwashambulia watuhumiwa hao, walilazimika kutimua mbio kuokoa maisha yao
baada ya kugeuziwa kibao na kuanza kushambuliwa.
Mkuu wa Wilaya ya
Missenyi, Denis Mwila alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka
wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi wanapowakamata watuhumiwa,
badala yake wawafikishe kwenye mikono ya vyombo vya dola kwa hatua za
kisheria.
Akizungumzia namna
njama za watuhumiwa hao zilivyojulikana na kuwanasa, Mkuu huyo wa wilaya
alisema uongozi wa kijiji na jeshi la polisi walipata taarifa kutoka kwa raia
wema kuhusu watu kutaka kuvamia nyumba ya mkazi huyo aliyeuza mifugo yake Mei
16. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema uchunguzi
kuhusu tukio hilo unaendelea na kuahidi kutoa taarifa baadaye.
|
No comments:
Post a Comment